Nov 11, 2020 08:17 UTC
  • Indhari ya Wazayuni kuhusu kusambaratika uchumi wa Israel

Naftali Bennett, kiongozi wa chama cha harakati ya mrengo wa kulia wenye kufurutu ada kinachojulikana kama chama cha The New Right amesema kuwa, katika hali ya hivi sasa Israel inaelekea upande hatari na wa kutisha na kwamba, imo mbioni kusambaratika kiuchumi.

Filihali utawala wa Kizayuni wa Israel unakabiliwa na matishio mbalimbali kama vile muundo wa kijamii usio na uwiano, tatizo la uhajiri na mgawanyikko wa kijami na kizazi. Hata hivyo, matatizo ya kiuchumi ndio changamoto kubwa inayoukabili utawala huo bandia. Uchumi wa utawala huo umekuwa ukidhoofika hatua kwa hatua katika miaka ya hivi karibuni na filahi umefikia katika hatua ya kusambaratika kabisa.

Kiwango cha ukosefu wa ajira katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepewa jina bandia la Israel kimeripotiwa kuongezeka mno hasa katika mwaka ulipota wa 2019 na mwaka huu unaoelekea ukingoni. Kanali ya Radio ya RTL ya Ufaransa imeandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Kiwango cha ukosefu wa ajira huko Israel katika miezi ya hivi karibuni kimepanda kutoka asilimia 3.4 mwezi Februari hadi asilimia 27 mwezi Aprili mwaka huu. Kiwango hicho cha ukosefu wa ajira kiliongezeka pia katika miezi iliyofuata.

Maandamano dhidi ya Benjamin Netanyahu

 

Aidha nakisi ya bajeti imeongezeka pia huko Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu). Baadhi ya asasi zimetabiri kwamba, nakisi ya bajeti ya Wazayuni itaongezeka kutokka asilimia 3.7 mwaka 2019 na kufikia asilimia 7 mwishoni mwa mwaka huu.

Kuna sababu mbalimbali zinazotajwa na wajuzi wa mambo kuhusiana na kuzorota uchumi wa utawala vamizi wa Israel.  Moja ya sababu hizo muhimu ni mlipuko wa virusi vya Corona katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Takwimu za hivi karibuni kabisa zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu 320,000 wameambukizwa virusi vya Corona. Baraza la Mawaziri la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu limekuwa na utendaji mbovu katika kukabiliana na mlipuko wa virusi vya Corona, kiasi kwamba, kumekuwa kukishuhudiwa maandamano mtawalia dhidi ya Israel ambapo waandamanaji wamekuwa wakitoa wito wa kujiuzulu Benjamin Netanyahu.

Kabla ya hapo, mtandao wa Kizayuni wa Walla ulikuwa umetangaza katika ripoti yake ukilinukuu Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba, kuenea virusi vya corona huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na matokeo yake mabaya kwa uchumi wa Israel kumepelekea kuongezeka kwa asilimia 40 kufilisika Wazayuni. Baraza la Mawaziri la Netanyahu linakabiliwa na matatizo ya  kiuchumi na kijamii katika kukabiliana na virusi vya corona. Tarehe 20 Machi mwaka huu, serikali ya Netanyahu ilipasisha sheria za hali ya tahadhari.

Matokeo ya sera hizi za kubana mambo si tu kwamba, hazijasaidia chochote katika kukabiliana na corona, bali zimeongeza matatizo ya kiuchumi kwa utawala huo.  

Mandamano ya wauguzi Israel wakilalamikia mazingira mabaya ya kazi

 

Ilan Baz mmoja wa maafisa usalama wa zamani wa Israel anasema kuhusiana na taathira za corona kwa uchumi wa utawala huo kwamba, uchumi wa Israel umepata pigo kubwa mno kutokana na kuenea virusi vya corona na zaidi ya wakazi wake milioni 1.2 hivi sasa hawana ajira.

Mbali na virusi vya corona, sera za Israel za kupenda vita ni sababu nyingine inayotajwa na weledi wa mambo kwamba, imechangia kuongeza matatizo ya utawala huo ghasibu. Katika muongo mmoja wa hivi karibuni ambapo madaraka yamekuwa mikononi mwa Benjamin Netanyahu, Israel imeanzisha vita katika miaka 2012, 2014, 2018 na 2019 dhidi ya Palestina. Licha ya kuwa, kwa vita vyake hivyo, Israel imewasababisha Wapalestina hasara mbalimbali, lakini yenyewe pia imegharamika pakubwa.

Kadhalika mipango ya kujipanua ya Israel katika ardhi za Wapalestina unazozikalia kwa mabavu kama ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi na kufuatilia mipango ya kumega ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuziunganisha na ardhi nyingine unazozikali kwa mabavu ni mambo ambayo yamepelekea kupungua kiwango cha usalama huko Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu), kwani makundi ya mapambano ya Palestina daima yamekuwa yakitoa majibu dhidi ya mipango hiyo na kusisitiza kusimama kidete dhidi ya mipango hiyo iliyojaa njama dhidi ya Wapalestina. Mjumuiko wa mambo haya kwa hakika umekuwa sababu ya kuongezeka matatizo ya kiuchumi na kuwafanya viongozi mbalimbali watahadharishe na kuonya kuhusiana na kusambaratika uchumi wa utawala huo ghasibu.

Tags