Wazayuni waendelea kuchimba mashimo na kubomoa Msikiti wa Al-Aqswa
(last modified Sat, 12 Dec 2020 02:59:02 GMT )
Dec 12, 2020 02:59 UTC
  • Wazayuni waendelea kuchimba mashimo na kubomoa Msikiti wa Al-Aqswa

Wazayuni wamekithirisha njama zao dhidi ya msikiti wa al-Aqswa kwa kuendelea kuchimba mashimo na njia za chini kwa chini kuelekea KATIKA msikiti huo mtakatifu ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.

Fakhri Abu Dibay, mtaalamu wa masuala ya Quds amesema kuwa, Wazayuni wameanza kubomoa na kuchimba mashimo na njia mpya za chini kwa chini kuelekea katika Msikiti huo mtakatifu hasa upande wa mashariki mwa msikitu huo.

Mtaalamu huyo wa masuala ya Quds amesema kuwa, eneo la mashariki mwa Msikiti wa al-Aqswa ambao Wazayuni wanachimba mashimo na njia za chini kwa chini ni la Ain al-Adhraa na kwamba, mashimo hayo sasa ni tishio kubwa kwa ukuta wa mashariki wa msikiti huo.

Wakati huo huo, baadhi ya ripoti zinasema kuwa, Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiwazuia Wapalestina kukarabati nyumba zao na umekuwa ukichimba kwa makusudi mashimo chini ya nyumba zao ili kuhatarisha uimara wa nyumba hizo na kisha kuwalazimisha Wapalestina hao wayahame makazi yao

Masjidul Aqswa

 

Itakumbukwa kuwa, tangu utawala dhalimu wa Israel ulipouvamia na kuanza kuukalia kwa mabavu mji mtakatifu wa Quds mwaka 1967 hadi sasa, umekuwa ukichimba mashimo ya chini ya ardhi katika mji huo hasa katika eneo lake la kale na kandokando mwa Msikiti wa Al-Aqswa ili kuwalazimisha Wapalestina wayahame maeneo hayo na kuweza kuyadhibiti maeneo yanayozunguka msikiti huo mtakatifu.

Lengo la utawala vamizi wa Israel la kuchimba mashimo ya njia za chini ya ardhi chini ya Msikiti wa Al-Aqswa ni kufuta nembo na athari za Kiislamu na za kihistoria za taifa la Palestina.