Hamas: Hujuma mpya ya Israel Ukanda wa Gaza itapata jibu kali
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i6553-hamas_hujuma_mpya_ya_israel_ukanda_wa_gaza_itapata_jibu_kali
Naibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ameuonya Utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mashambulizi yake mapya katika Ukanda wa Gaza huku uvamizi huo mpya wa Tel Aviv katika eneo hilo ukiingia siku yake ya nne Jumamosi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 06, 2016 23:50 UTC
  • Hamas: Hujuma mpya ya Israel Ukanda wa Gaza itapata jibu kali

Naibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ameuonya Utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mashambulizi yake mapya katika Ukanda wa Gaza huku uvamizi huo mpya wa Tel Aviv katika eneo hilo ukiingia siku yake ya nne Jumamosi.

Katika hotuba yake ya jana Ijumaa, Islamail Haniya ambaye pia ni Mkuu wa Hamas katika Ukanda wa Gaza amesema harakati hiyo ya muqawama itatoa jibu kali kwa chokochoko za Utawala Haramu wa Israel.

Amesema: "Hamas haikua na nia ya kuingia katika vita vipya na Israel miaka miwili baada ya mashambulizi ya utawala huo wa Kizayuni kusababisha hasara kubwa katika ukanda huo, lakini katu hatutaruhusu uchokozi huo uendelee."

Jana Ijumaa jeshi la Utawala wa Kizayuni lilitoa taarifa na kueleza kuwa kwa mara ya kwanza tangu vita vya siku 50 vya mwaka 2014, wanapambano wa Hamas na askari wa jeshi hilo wamepambana ana kwa ana katika eneo hilo.

Siku ya Jumatano, askari wa Utawala haramu wa Kizayuni walishambulia maeneo ya mpakani mwa Ukanda wa Gaza ambapo katika kujibu hujuma hiyo, wanamuqawama wa Palestina walipambana na askari hao.

Mashambulio yanayoendelea kufanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza ni ukiukaji wa makubaliano ya usitishaji vita yaliyofikiwa baina ya pande mbili mwezi Agosti mwaka 2014 baada ya vita vya siku 50, ambapo utawala haramu wa Israel uliwaua shahidi zaidi ya Wapalestina 2,300 wakiwemo wanawake na watoto na kuwajeruhi maelfu ya wengine.