Madola vamizi yazidi kuiba mafuta ya wananchi maskini wa Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i65806-madola_vamizi_yazidi_kuiba_mafuta_ya_wananchi_maskini_wa_yemen
Duru za usalama za Yemen zimetangaza kuwa, madola vamizi yanayoongozwa na Saudi Arabia na Imarati yanaendelea kuiba mafuta ya nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 17, 2021 02:20 UTC
  • Madola vamizi yazidi kuiba mafuta ya wananchi maskini wa Yemen

Duru za usalama za Yemen zimetangaza kuwa, madola vamizi yanayoongozwa na Saudi Arabia na Imarati yanaendelea kuiba mafuta ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Shirika la habari la Yemen, SABA, limemnukuu Naibu Mkuu wa Mkoa wa Shabwah akisema hayo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, dola vamizi la Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) mbali na kuongeza kina cha visima vilivyopo, limechimba visima vingine vingi vya mafuta katika eneo la al Qasha'ah la mkoa huo.

Al Risas Hussein al Bakri amelalamikia pia magendo ya mafuta yanayosafirishwa nje ya Yemen kupitia bandari ya Qana yanayofanywa na mamluki wa dola vamizi la Saudia na kusema kuwa, magendo ya mafuta yanaendelea kama kawaida katika bandari hiyo.

Katika moja ya bandari za Yemen

 

Afisa huyo mwandamizi wa Yemen amesisitiza kuwa, wavamizi na mamluki wao wanahakikisha kuwa vita havimaliziki baina ya makabila mbalimbali ikiwa ni sehemu muhimu ya kuendesha siasa na jinai zao pamoja na kuhakikisha wananchi wa Yemen wanaendelea kuwa maskini licha ya utajiri mkubwa wa maliasili wa nchi yao.

Baada ya hapo ametoa mwito kwa makabila yote ya Yemen kuwa macho mbele ya siasa na mipango hiyo ya kijinai ya wavamizi wa nchi yao akisisitiza kuwa, wavamizi hao hawana kheri yoyote kwa taifa lao zaidi ya kufanya jinai na kupora utajiri wake.

Saudi Arabia imejenga bomba maalumu la kuibia mafuta ya Yemen. Bomba hilo linatokea eneo la kaskazini mwa mkoa wa Hadhramout hadi Saudia na limejengwa na kusimamiwa na shirika la mafuta la Saudi Arabia, ARAMCO.