Kufunguliwa ubalozi; Imarati katika mkondo wa kupanua uhusiano na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i66138-kufunguliwa_ubalozi_imarati_katika_mkondo_wa_kupanua_uhusiano_na_israel
Ubalozi wa utawala haramu wa Israel ulifunguliwa rasmi huko Abu Dhabi mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) tarehe 21 ya mwezi huu wa Januari.
(last modified 2026-01-03T13:29:21+00:00 )
Jan 27, 2021 02:41 UTC
  • Kufunguliwa ubalozi; Imarati katika mkondo wa kupanua uhusiano na Israel

Ubalozi wa utawala haramu wa Israel ulifunguliwa rasmi huko Abu Dhabi mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) tarehe 21 ya mwezi huu wa Januari.

Nalo Baraza la Mawaziri la Imarati Jumapili ya juzi liliafiki kufunguliwa ubalozi wa nchi hiyo huko Tel Aviv. Kuanzia Septemba 20 mwaka jana (2020) nchi nne za Kiarabu za Imarati, Sudan, Bahrain na Morocco zilitia saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ilikuwa nchi ya kwanza kati ya nchi hizo nne kutangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ambayo inatenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi wa Palestina. Ilikuwa tarehe 15 Septemba mwaka jana wakati Imarati ilipotiliana saini makubaliano na Israel ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina yao.

Tangu kutiwa saini makubaliano hayo na kuanza rasmi uhusiano baina ya pande mbili, tayari kumefanyika mambo kadhaa kama kuanza safari za ndege za moja kwa moja baina ya Imarati na Israel huku kukiwemo na safari ya jumbe za kibiashara kati ya pande mbili hizo. Kadhalika katika kipindi hiki, maelfu ya watalii wa Israel wamefanya safari nchini Imarati. Mbali na Imarati kufungua rasmi ubalozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mjini Abu Dhabi, nchi hiyo ya Kiarabu ina mpango wa kuhakikisha kunafunguliwa pia ubalozi mdogo wa Israel katika jiji la kimataifa la Dubai.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Imarati, Bahrain na utawala haramu wa Israel wakionyesha nyaraka baada ya kutiliana saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano baina yao kwa usimizi wa Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump. hafla hiyo ilifanyika katika Ikulu ya Marekani White House

 

Matukio hayo kwa hakika yanaonesha kuwa, filihali Imarati inalipa kipaumbele na kuzingatia mno suala la kupanua uhusiano wake na Israel na imekuwa ikichukua hatua moja baada ya nyingine kwa minajili ya kufikia malengo mbalimbali katika uwanja huo.

Licha ya kuwa, diplomasia ya serikali ya zamani ya Marekani chini ya uongozi wa Donald Trump  ilikuwa na taathira kwa nchi za Kiarabu ikiwemo Imarati kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel, lakini tawala za Manama na Abu Dhabi kinyume na Sudan na Morocco na kutokana na sababu tofauti tofauti, zenyewe zilikuwa na utayari wa lazima wa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo ghasibu.

Licha ya kuwa, Imarati ni mshirika mkuu wa Saudi Arabia katika vita dhidi ya Yemen, lakini Abu Dhabi imekuwa na ushindani wa siri na wa dhahiri na Riyadh kwa ajili ya kuwa na satua na ushawishi katika eneo. Imarati kupitia kuanzisha kwake uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel imo mbioni kuondoka katika kivuli cha Saudia kwa upande mmoja, na ipate himaya na uungaji mkono wa Israel kuhusiana na masuala mbalimbali ya Asia Mgharibi kwa upande wa pili.

 

Hii ni katika hali ambayo, Israel hususan katika miaka miwili ya hivi karibuni, iko hoi bin taabani kutokana na kukabiliwa na migogoro lukuki ya ndani, ambapo kwa zaidi ya majuma 31 sasa wananchi wa Israel wamekuwa wakiandamana wakitaka Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo ajiuzulu na kung'atuka katika ulingo wa siasa. Aidha Israel kutokana na kuandamwa na kirusi cha mizozo na migawanyiko ya kisiasa, hivi sasa inajiandaa na uchaguzi wa nne wa Bunge katika kipindi cha miaka miwili, uchaguzi ambao umepangwa kufanyika mwezi Machi mwaka huu.

Jambo jingine ni kuwa, serikali ya Imarati imechukua uamuzi wa kufungua ubalozi wa Israel huko Abu Dhabi na kuafiki kufungua ubalozi wake huko Tel Aviv katika kipindi hiki cha siku za mwanzo za kuanza kipindi cha uongozi wa Rais Joe Biden nchini Marekani. Kwa msingi huo, inawezekana kusema kuwa, uamuzi huu wa Imarati unalenga kutafuta ridhaa na himaya ya serikali mpya ya Marekani chini ya uongozi wa Biden na kwa namna fulani kufikisha ujumbe huu kwamba, Abu Dhabi haina wasiwasi na kuondolewa madarakani Donald Trump.

 

Jambo jingine ni hili kwamba, Imarati inasukuma mbele gurudumu la kupanua uhusiano na Israel katika kivuli cha ukandamizaji wa ndani na kuzusha hofu na wahaka dhidi ya kila anayepingana na siasa hizi. Licha ya kuwa Imarati ina muundo wa kijamii usio na uwiano, lakini fikra za waliowengi nchini humo kama ilivyo katika mataifa mengine ya Kiarabu zinapinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Baada ya kutiwa saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano na utawala wa kigaidi wa Israel, Wizara ya Kusukuma Mbele Mikakati ya Israel ilitangaza katika ripoti yake kwamba, asilimia 90 ya gumzo na mijadala ya Kiarabu katika ulimwengu wa Kiarabu katika mitandao ya kijamii inapinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel.

Katika fremu hiyo, Hamad al-Shamsi, mwanaharakati wa kisiasa wa Imarati anayeishi nchini Uturuki anasema: Kila anayepinga mchakato wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Imarati na uatawala ghasibu wa Israel, yumkini akakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 10 jela na faini ya hadi dirihamu milioni moja. Aidha anaongeza kuwa, wafuasi wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ni wachache mno na utawala wa Imarati umekuwa ukiwatumia na kunufaika nao kwa ajili ya kuidhinisha misimamo yake yote katika uga wa masuala ya kigeni.