Wasiwasi wa UN wa kuendelea kuteswa wanaharakati katika jela za Imarati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i66762-wasiwasi_wa_un_wa_kuendelea_kuteswa_wanaharakati_katika_jela_za_imarati
Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Haki za Binadamu ameelezea kusikitishwa na hali mbaya na mateso wanayofanyiwa wanaharakati wa haki za binadamu katika jela za Umoja wa Falme za Kiarabu na ametaka waachiliwe huru.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 12, 2021 07:40 UTC
  • Wasiwasi wa UN wa kuendelea kuteswa wanaharakati katika jela za Imarati

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Haki za Binadamu ameelezea kusikitishwa na hali mbaya na mateso wanayofanyiwa wanaharakati wa haki za binadamu katika jela za Umoja wa Falme za Kiarabu na ametaka waachiliwe huru.

Mtandao wa Arabi 21 umemnukuu Mary Lawlor akisema katika tamko maalumu kwamba hali ya wanaharakati wa haki za binadamu nchini Imarati ni mbaya na amewataka viongozi wa nchi hiyo kuwaachilia huru wanaharakati hao hasa wale waliopitisha muda mrefu korokoroni na ambao kuna hofu kwamba wanapewa mateso makali na kutendewa vitendo viovu huko wanakoshikiliwa.

Ripota huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Haki za Binadamu vile vile amesema katika taarifa yake kwamba Mohammed Abdullah al Rukn, Ahmad Mansour na Naser bin Ghaith, ni wanasheria watatu waliotiwa jela kutokana na kutumia haki yao ya kisheria na bila ya kuchochea machafuko. Amesema, wanaharakati hao wako katika jela za Umoja wa Falme za Kiarabu kwa miaka 10 sasa na wanateswa na kutendewa vitendo vibaya huko wanakoshikiliwa.

Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) unashutumiwa kwa kuwatesa vibaya wafungwa

 

Kwa miaka kadhaa sasa Imarati inashutumiwa vikali na duru na pande mbalimbali kutokana na kuwatia nguvuni na kuwaweka korokoroni mamia ya wanaharakati wa haki za binadamu kwa kutumia haki yao ya kutaka marekebisho ya kisiasa na kuitishwa chaguzi za kidemokrasia nchini humo.

Ripoti nyingi za kimtaifa zinaonesha kuwa, hali ya jela za Umoja wa Falme za Kiarabu ni mbaya. Ni jambo la kawaida kabisa kuteswa vibaya wafungwa katika jela hizo kiasi kwamba baadhi ya wafungwa wanapoteza maisha kwa mateso au wengine wanaamua kujiua kwa kushindwa kuhimili mateso na unyanyasaji mkubwa wanaofanyiwa.