Askari wa Kizayuni wawaua shahidi Wapalestina watatu katika Ukanda wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i67624-askari_wa_kizayuni_wawaua_shahidi_wapalestina_watatu_katika_ukanda_wa_gaza
Askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wamewaua shahidi wavuvi watatu Wapalestina baada ya kuifyatulia kombora boti yao ya uvuvi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 07, 2021 10:26 UTC
  • Askari wa Kizayuni wawaua shahidi Wapalestina watatu katika Ukanda wa Gaza

Askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wamewaua shahidi wavuvi watatu Wapalestina baada ya kuifyatulia kombora boti yao ya uvuvi.

Kanali ya televisheni ya Al Mayadin imeripoti kuwa, askari wa jeshi la utawala ghasibu wa Kizayuni waliishambulia boti hiyo ya uvuvi leo asubuhi karibu na pwani ya eneo la Khun Yunes.

Askari wa jeshi la majini la utawala haramu wa Israel wameshawahi kuwashambulia mara kadhaa kwa silaha wavuvi Wapalestina wa eneo la Ukanda wa Gaza, ambapo makumi ya Wapalestina wameuawa na kujeruhiwa katika hujuma hizo za Wazayuni.

Mnamo katikati ya msimu wa joto wa mwaka uliopita, na kufuatia kushadidi mivutano katika mipaka ya Ukanda wa Gaza na maeneo mengine ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, utawala wa Kizayuni ulitangaza kulifunga kwa muda usiojulikana eneo la bahari la Gaza linalotumiwa na Wapalestina kwa ajili ya shughuli za uvuvi.

Hali duni ya kimaisha katika Ukanda wa Gaza ulioathiriwa na mzingiro wa Israel

Hatua hiyo ya kinyama imechukuliwa wakati eneo la Ukanda wa Gaza lingali linakabiliwa na matatizo ya kiuchumi na kimaisha kutokana na mzingiro unaoendelea kwa mwaka wa 14 sasa liliowekewa na utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel.

Maelfu ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wanategemea uvuvi kwa ajili ya kujipatia kipato cha kukimu mahitaji yao ya kila siku na bila kuvua samaki hushindwa kujimudu kimaisha.../