Kamanda mwandamizi wa Daesh auawa nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i6793-kamanda_mwandamizi_wa_daesh_auawa_nchini_iraq
Kamanda mwandamizi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ameuawa katika hujuma ya anga nchini Iraq. Haya yanajiri huku wanajeshi wa Iraq na makundi ya wanamgambo waitifaki wakifanikiwa kukomboa vijiji kadhaa vya mkoa wa Anbar, magharibi mwa nchi hiyo ambavyo vimekuwa vikishikiliwa na magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 10, 2016 07:50 UTC
  •  Kamanda mwandamizi wa Daesh auawa nchini Iraq

Kamanda mwandamizi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ameuawa katika hujuma ya anga nchini Iraq. Haya yanajiri huku wanajeshi wa Iraq na makundi ya wanamgambo waitifaki wakifanikiwa kukomboa vijiji kadhaa vya mkoa wa Anbar, magharibi mwa nchi hiyo ambavyo vimekuwa vikishikiliwa na magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imethibitisha habari za kuuawa Abu Wahib, ambaye pia anajulikana kama Shakir Wahib pamoja wenzake watatu katika shambulio la anga karibu na mji wa Rutbah mkoani Anbar.

Peter Cook, Msemaji wa Pentagon amesema Abu Wahib ambaye amekuwa akionekana kwenye kanda za video akichinja mateka wao ameuawa pamoja na wanachama wengine wa kundi hilo la kigaidi.

Imearifiwa kuwa, gaidi huyo mwandamizi wa Daesh aliwahi kukamatwa nchini Iraq mwaka 2006 na kisha kuhukumiwa kifo, lakini akatoroka gerezani mwaka 2012.

Maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Iraq ukimweo mkoa wa Anbar yamekuwa yakishuhudia wimbi la mashambulizi ya kigaidi kutoka kundi la Daesh, tangu lilipoanzisha hujuma zake za kinyama mwezi Juni mwaka 2014.

Katika ripoti yake ya kila mwezi Jumapili iliyopita, Umoja wa Mataifa ulisema zaidi ya watu 700 wameuawa mwezi uliopita wa Aprili pekee nchini Iraq.