Mar 18, 2021 13:17 UTC
  • Rais wa Iraq asisitiza kuhusu askari wa Marekani kuondoka nchini humo

Rais Barham Salih wa Iraq ametangaza kuwa, uamuzi umeshachukuliwa kuhusu kuhitimisha kuwepo kwa vikosi vya jeshi vamizi la Marekani nchini humo.

Barham Salih ametangaza leo Alkhamisi kuwa, uamuzi umeshachukuliwa kuhusu kuhitimisha kuwepo kwa vikosi vya jeshi la Marekani na majeshi mengine ya kigeni nchini Iraq na kwamba kwa hivi sasa idadi ya askari hao haizidi elfu mbili na mia tano.

Rais wa Iraq ameashiria pia ombwe lililojitokeza katika uhusiano wa serikali kuu ya Iraq na eneo la Kurdistan ambalo ni sehemu ya ardhi ya nchi hiyo inayojiendeshea mambo yake na akasema, kuna udharura wa uhusiano huo kufuata mkondo sahihi na kufanyika mazungumzo ya kitaifa ya kuwezesha kila upande kutambua haki na wajibu wake.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Shirika la Kijeshi la NATO, Jens Stoltenberg alisema kuwa, shirika hilo linataka kuongeza idadi ya askari wake walioko Iraq kutoka mia tano hadi elfu nne.

Jens Stoltenberg

Askari wa jeshi vamizi la Marekani wamepiga kambi nchini Iraq tangu mwaka 2003, wakati wananchi na makundi mbali mbali ya Iraq yameshapaza sauti mara kadhaa kutaka askari hao waondoke, huku bunge la Iraq likiwa limeshapitisha mpango tangu Januari mwaka 2020 kuhusiana na kuondoka askari hao katika ardhi ya nchi hiyo.../

Tags