Yemen: UN ni mshirika katika uharamia wa Saudia na washirika wake
(last modified Sat, 17 Apr 2021 08:20:29 GMT )
Apr 17, 2021 08:20 UTC
  • Yemen: UN ni mshirika katika uharamia wa Saudia na washirika wake

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mafuta la Yemen amekosoa hatua ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia wa kuendelea kushikilia meli zinazobeba mafuta kuelekea Yemen na kusema kuwa Umoja wa Mataifa pia ni mshirika katika uharamia huo.

Ammar al Adh'rai' amesema kuwa, Saudi Arabia na washirika wake wakiongozwa na Marekani wanaendelea kushikilia meli zinazobeba mafuta zinazoelekea kwenye bandari za Yemen na kwamba, tangu mwanzoni mwa mwaka huu meli moja tu ya mafuta ndiyo iliyotia nanga katika Bandari ya Al Hudaydah. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mafuta la Yemen amesema kuwa, maisha ya Wayemeni milioni 26 yatakuwa hatarini iwapo Saudia na washirika wake wataendelea kuzuia meli zinazobeba mafuta kutia nanga katika bandari ya al Hudaydah.

Watoto wa Yemen

Awali afisa huyo wa Yemen alikuwa amesema kuwa, hasara zilizosababishwa na uharamia huo wa Saudia na Marekani dhidi ya taifa la Yemen tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2021 pekee zimefikia dola milioni 34 na nusu. 

Muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya taifa la Yemen unaizingira nchi hiyo baharini, nchini kavu na angani na hauruhusu meli zinazobeba bidhaa muhimu kama chakula, dawa na mafuta kutia nanga katika bandari za Yemen kwa karibu miaka 7 sasa. 

Wakati huo huo ripoti za mashirika ya kimataifa zinasema kuwa mamilioni ya Wayemeni wakabiliwa na baa la njaa. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinasema kuwa, nchi hiyo inasumbuliwa na maafa makubwa zaidi ya binadamu dunia katik kipindi cha sasa.