Kituo cha MOSSAD chashambuliwa Erbil huku Waziri wa Israel akiitembelea UAE
Huku Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa utawala haramu wa Israel akifanya safari ya kwanza ya kuutembelea Umoja wa Falme za Kiarabu, kambi ya Shirika la Kijasusi la Utawala huo wa Kizayuni (MOSSAD) imeshambuliwa kwa maroketi katika eneo la Erbil, kaskazini mwa Iraq.
Duru za habari zinaarifu kuwa, maajenti kadhaa wa utawala haramu wa Israel wameangamizwa huku wengine wakijeruhiwa katika shambulio hilo la Erbil.
Hata hivyo hadi tunamaliza kuandaa taarifa hii, Tel Aviv na Erbil hazikuwa zimetoa taarifa yoyote kuhusu shambulio hilo dhidi ya kambi ya majasusi wa MOSSAD.
Shambulio hilo limejiri huku Yair Lapid, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel akiitembelea UAE, ambapo amefungua rasmi ubalozi wa utawala huo wa Kizayuni katika mji mkuu Abu Dhabi, na pia ubalozi mdogo wa utawala huo pandikizi mjini Dubai, licha ya kuanza kufanya kazi miezi mitano iliyopita.
Mapema mwezi huu, Imarati ilifungua rasmi ubalozi wake mjini Tel Aviv, siku chache tu baada ya dunia kushuhudia jinai na mauaji ya kutisha ya zaidi ya Wapalestina 250 wa Ukanda wa Gaza, yaliyofanywa na jeshi katili la Israel.
Umoja wa Falme za Kiarabu Septemba mwaka jana ilianzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel, ikiwa ni nchi ya kwanza ya Kiarabu jkufanya hivyo baada ya kipindi cha miaka 26. Baadhi ya tawala za Kiarabu kama Sudan, Bahrain na Morocco zimefuata mkumbo huo kibubusa.