Imarati yapiga marufuku raia wake kutembelea nchi 8 za Afrika
Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) umewataka raia wake wasitembelee nchi 14 duniani nyingi zake zikiwa ni za barani Afrika kwa madai ya kuenea maambukizo ya kirusi cha corona.
Vyombo vya habari vimeinukuu wizara ya mambo ya nje ya Imarati ikitoa tangazo hilo jana Alkhamisi na kuwataka raia wake wasitembelee nchi 14 duniani hadi litakapotoka tangazo jingine. Nchi hizo 8 ni za Afrika na sita ni za barani Asia.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Imarati imezitaja nchi hizo kuwa ni India, Pakistan, Bangladesh, Nepal, Sri Lanka na Vietman kwa upande wa barani Asia; na Namibia, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrsia ya Congo, Uganda, Sierra Leone, Liberia, Afrika Kusini na Nigeria kwa upande wa Afrika.
Maafisa wa ofisi za kibalozi za Umoja wa Falme za Kiarabu zilizoko katika nchi hizo pamoja na masuala kama matibabu ya dharura, wajumbe rasmi wa kiuchumi na kielimu, hawamo kwenye marufuku hiyo. Nchi hiyo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi aidha imewataka raia wake wachunge masharti na maelekezo yote ya watu wa afya kuhusiana na kujikinga na ugonjwa wa corona au COVID-19.
Virusi vipya vya corona vilivyogunduliwa nchini Uingereza, Afrika Kusini na India vimepelekea kuongezeka maambukizo ya ugonjwa wa corona na wagonjwa wa COVID-19 katika pembe zote za dunia. Idadi ya watu wanaopoteza maisha kwa ugonjwa huo pia wanaongezeka siku baada ya siku na kusababisha wasiwasi mkubwa katika kona mbalimbali za dunia.
Hayo yameripotiwa huku Shirika la Afya Duniani WHO likitangaza kuwa, idadi ya watu walioambukizwa kirusi cha corona barani Ulaya imeongezeka tena baada ya wiki kumi za kupungua kwake.