Utawala wa Israel wajeruhi waandamanaji 150 Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71934-utawala_wa_israel_wajeruhi_waandamanaji_150_wapalestina_katika_ukingo_wa_magharibi
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewahujumu Wapalestina waliokuwa wakiandamana kwa amani dhidi ya ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika mji wa Nablus ulio katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Jul 03, 2021 03:17 UTC
  • Utawala wa Israel wajeruhi waandamanaji 150 Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewahujumu Wapalestina waliokuwa wakiandamana kwa amani dhidi ya ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika mji wa Nablus ulio katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Duru zinaarifu kuwa baada ya Sala ya Ijumaa, wanajeshi wa utawala dhalimu wa Israel waliwashambulia Wapalestina waliokuwa wakiandamana dhidi ya ujenzi wa kitongoji cha Eviatar katika eneo la Jabal Sabih mjini Beita.

Shirika rasmi la habari la Palestina , WAFA, limeandika kuwa wanajeshi wa utawala haramu wa Israel walitumia risasi za plastiki kuwatawanya waandamanaji ambapo, Wapalestina 150 waliokuwa wakiandamana kwa amani wamejeruhiwa na saba miongoni mwao wamelazwa hospitalini.

Kitongoji haramu cha Eviatar kimekuwa kitovu cha mvutano baina ya Wazayuni na Wapalestina.  Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanautaka utawala wa Israel utekeleze amri ya mahakama ambayo imetaka walowezi wa Kizayuni waondolewe katika kitongoji hicho.

Buldoza La utawala haramu wa Israel zikibomoa nyumba za Wapalestina ili kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

Desemba 23, 2016 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio 2334 ambalo liliutaka utawala haramu wa Israel usimamishe haraka na kikamilifu shughuli zote za ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kwa kuyazayunisha maeneo hayo, uhakikishe unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.