Imarati yatakiwa iwaachie huru makumi ya wanaharakati wa kisiasa
Shirika moja la kutetea haki za binadamu lenye makao yake nchini Uingereza limeeleza wasi wasi wake juu ya kukandamizwa kwa wanaharakati wa haki za binadamu na jinsi wanavyoteswa wakiwa magerezani katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Katika barua yake kwa Balozi wa Imarati nchini Uingereza, Mansoor Abulhoul, shirika hilo la 'International Campaign for Freedom in the United Arab Emirates' (ICFUAE) limeitaka Abu Dhabi iwaachie huru wafungwa 94 wa kisiasa, ambao wanazuiliwa kwa mwaka wa nane sasa katika magereza ya kugofya ya UAE.
Barua hiyo imeeleza kuwa, baadhi ya wafungwa hao wana alama za kuteswa zilizo wazi katika miili yao, walizozipata kutokana na ukatili waliofanyiwa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya Kiarabu wakiwa kizuizini, hata kabla ya kufunguliwa mashitaka.
Shirika hilo la UK limezikosoa vikali mamlaka za Imarati kwa kufeli kuagiza kufanyika uchunguzi wa kukamatwa na kuhukumiwa kwa makundi wanaharakati hao, na vile vile juu ya ukandamizaji wanaofanyiwa wakiwa korokoroni na magerezani.
ICFUAE imebainisha kuwa, baadhi ya mbinu za mateso zinazotumiwa na maafisa wa Imarati dhidi ya watetezi wa haki za binadamu na wafungwa wa kisiasa ni kuwazuia watu wa familia za wanaharakati hao ama kuingia au kutoka nje ya nchi.
Julai 2 mwaka 2013, mahakama moja huko Imarati iliwatolea hukumu ya pamoja na kuwafunga jela akthari ya wafungwa hao wanaofahamika kama 'UAE 94' baada ya kubambikiwa madai kuwa walipanga kufanya mapinduzi.