Yemen yakosoa Imarati na Israel kukalia kwa mabavu kisiwa cha Mayyun
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i73914-yemen_yakosoa_imarati_na_israel_kukalia_kwa_mabavu_kisiwa_cha_mayyun
Afisa wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema lengo la Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel kukikalia kwa mabavu kisiwa cha Mayyun kilichoko katika Lango Bahari la Mandab kusini mwa Bahari Nyekundu ni kukidhibiti kutokana na nafasi yake muhimu kijiografia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 25, 2021 12:56 UTC
  • Yemen yakosoa Imarati na Israel kukalia kwa mabavu kisiwa cha Mayyun

Afisa wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema lengo la Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel kukikalia kwa mabavu kisiwa cha Mayyun kilichoko katika Lango Bahari la Mandab kusini mwa Bahari Nyekundu ni kukidhibiti kutokana na nafasi yake muhimu kijiografia.

Ahmed al-Rahwi ameiambia kanali ya televisheni ya al-Masira kuwa, shabaha ya kufurushwa kwa nguvu wakazi wa kisiwa hicho ambacho kinafahamika pia kama Perim ni kutaka kuidhibiti njia hiyo muhimu ya baharini.

Amesema, "katika miaka ya hivi karibuni, UAE imeshadidisha hatua ya kuwafukuza wakazi wa kisiwa hicho ili iunde kambi ya kijeshi, kwa amri ya Marekani na Israel."

Afisa huyu mwandamizi wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema muungano vamizi unapaswa kujifunza kutokana na matukio ya huko nyuma, na kusisitiza kuwa wananchi wa Yemen kwa mara nyingine wataonesha nguvu zao katika kukabiliana na wavamizi. 

Kisiwa cha Socotra cha Yemen kinachokaliwa kwa mabavu na muungano vamizi

Julai mwaka jana, wanajeshi wa Imarati walikikalia kwa mabavu kisiwa kingine cha Socotra huko kusini mwa Yemen, baada ya kushtadi mapigano kati ya wanajeshi wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen ya Abdu Rabb Mansour Hadi wanaoungwa mkono na Saudi Arabia na Baraza la Mpito la kusini mwa Yemen.  

Raia wa Yemen wanaoishi katika kisiwa cha Socotra wameshafanya maandamano mara kadhaa kulalamikia uwepo wa wanajeshi wa Imarati kisiwani humo.