Iraq: Tarehe ya kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini haibadilishiki
(last modified 2021-11-28T02:50:59+00:00 )
Nov 28, 2021 02:50 UTC
  • Iraq: Tarehe ya kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini haibadilishiki

Msemaji wa Komandi ya Operesheni za Pamoja ya Iraq amesema kuwa, wakati wa kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini humo haibadilishiki.

Meja Jenerali Tahsin al Khafaji alisema hayo jana na kuongeza kuwa wakati uliokubaliwa wa kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ni sehemu muhimu ya makubaliano ya kiusalama baina ya nchi hizo mbili na tarehe hiyo haiwezi kubadilishwa kabisa. 

Amesema, uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Iraq unamalizika mwishoni mwa mwaka huu wa 2021, baada ya hapo maafisa wa kijeshi wa Marekani watakaobakia nchini humo watakuwa ni washauri na walimu tu wa mafunzo ya kijeshi. 

Matamshi hayo ya Msemaji wa Komandi ya Operesheni za Pamoja ya Iraq yamekuja baada ya makundi ya kisiasa nchini nchini humo kusema kuwa, Marekani inaendelea kufanya njama za kuchochea machafuko na umwagaji damu ili kujiwekea kinga ya kutotimuliwa nchini Iraq.

Wanajeshi wa Marekani

 

Juzi tovuti ya habari ya al Maaluma ilimnukuu Faris Shakir, mjumbe wa muungano wa Fat'h nchini Iraq akisema kuwa, Marekani inaendesha njama za kuzusha fitna, machafuko na mauaji nchini humo ili kushinikiza kubakia wanajeshi wake na kuhakikisha kila anayepigania kutimuliwa wanajeshi magaidi wa Marekani huko Iraq, anatengwa.

Naye Mohammad al Sahyud, mjumbe wa muungano wa Serikali ya Sheria nchini Iraq amesema, Iraq hivi sasa haihitaji tena kuweko wanajeshi wa Marekani na kila mmoja anajua vyema uamuzi wa Bunge na makubaliano ya kutimuliwa wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2021. Kwa kweli hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha kuendelea kuweko wanajeshi wa Marekani nchini Iraq.

Tags