EuroMed Rights: Zaidi ya nusu ya watu wa Gaza ni maskini
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i79616-euromed_rights_zaidi_ya_nusu_ya_watu_wa_gaza_ni_maskini
Shirika moja la kutetea haki za binadamu limesema, zaidi ya nusu ya watu wa Ukanda wa Gaza wanasumbuliwa na umaskini uliokithiri kutokana na mzingiro wa kiuchumi wa miaka 16 uliowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 26, 2022 00:42 UTC
  • EuroMed Rights: Zaidi ya nusu ya watu wa Gaza ni maskini

Shirika moja la kutetea haki za binadamu limesema, zaidi ya nusu ya watu wa Ukanda wa Gaza wanasumbuliwa na umaskini uliokithiri kutokana na mzingiro wa kiuchumi wa miaka 16 uliowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ripoti iliyotolewa na taasisi ya kutetea haki za binadamu ya Ulaya, Euro-Mediterranean Human Rights Watch, imeeleza kuwa takriban watu milioni 1.5 katika Ukanda wa Gaza wanaishi chini ya mstari wa umaskini kutokana na mzingiro na vikwazo vilivyowekwa na utawala wa Kizayuni tangu mwaka 2006. 

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kuishinikiza Israel ili ikomeshe mzingiro wake haramu dhidi ya watu wa Gaza.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, siasa za Israel za kutoa adhabu na kuwatesa kwa halaiki wakazi wa Ukanda wa Gaza zinaendelea, na zinaonyesha wazi nia ya utawala huo ya kuwasababishia uharibifu mkubwa wa kimaada na kimaadili wakazi wa eneo hilo.

Ripoti ya shirika la haki za binadamu la EuroMed Rights inaonyesha kuwa, kiwango cha ukosefu wa ajira katika Ukanda wa Gaza kimeongezeka kutoka asilimia 23.6 mwaka 2005 hadi asilimia 50.2 mwishoni mwa 2021.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, hali ya Gaza inaporomoka, kwa sababu taasisi za kiuchumi, huduma na uzalishaji zimeharibiwa wakati wa mashambulizi ya kipindi cha mzingiro wa Israel; kiasi kwamba katika vita vya hivi majuzi vya Israel na Hamas pekee, Ukanda wa Gaza umepata hasara ya zaidi ya dola milioni 40.

Mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa gaza

Eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina limekuwa chini ya mzingiro wa nchi kavu, anga na baharini wa Israel tangu mwaka 2006, na wakazi wake wanasumbiliwa na matatizo mengi.