Wazayuni waendeleza uvamizi dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameendeleza uhasama wao na kwa mara nyingine wameuvamia Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem).
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Palestina la Shahab, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mapema Alhamisi waliuvamia Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Katika hujuma hiyo wanajeshi wa Israel walikabiliana na vijana Wapalestina ambao walikuwa wanaulinda msikiti huo.
Baada ya makabiliano hayo askari wa utawala haramu wa Israel waliwakamata vijana kadhaa Wapalestina.
Jumatano usiku pia wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walikabiliana na vijana Wapalestina katika kitongoji cha Al Tur huko Quds Mashariki ambapo vijana hao walilazimisha gari la jeshi la Kizayuni kutoroka eneo hilo.
Msikiti wa al-Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu umekuwa ukiandamwa na njama mtawalia za utawala vamizi wa Israel, hatua ambazo zinakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.
Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kuyazayunisha maeneo hayo na kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.