Amnesty: Israel inatekeleza jinai ya ‘apartheid’ dhidi ya Wapalestina
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa mwito wa kubebeshwa dhima utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa hatua yake ya kutumia mfumo wa kibaguzi wa apartheid dhidi ya wananchi wa Palestina.
Amnesty imesema hayo leo Jumanne katika kikao na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, utawala haramu wa Israel unatumia mbinu za apartheid kwa kuwakandamiza na kuwatesa Wapalestina, sanjari na kukanyaga haki zao za msingi.
Taarifa ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini London, Uingereza imeeleza kuwa, Israel inawafanyia jinai hizo Wapalestina hususan katika Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds Mashariki.
Amnesty International imeeleza bayana kuwa, kupokonywa ardhi, kobomolewa nyumba, kuuawa kinyume cha sheria, kuvuliwa uraia, kufungwa na kuteswa ni sehemu ya mbinu za mfumo wa apartheid unaotumiwa na Tel Aviv dhidi ya Wapalestina.
Shirika hilo limetoa mwito kwa jamii ya kimataifa hususan Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kuwafuatilia na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wa jinai hizo za mfumo wa apartheid dhidi ya wananchi wa Palestina.