Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wiki ijayo kuelekea Qatar
Balozi wa Iran mjini Doha, Qatar ametoa maelezo kuhusu ziara tarajiwa ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini humo.
Gazeti la al Quds al Arabi limezinukuu duru za kidiplomasia za Qatar na kutangaza kuwa, Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Alhamisi wiki hii ataelekea nchini Qatar kwa mashauriano na viongozi wa nchi hiyo kuhusu masuala ya kieneo na faili la nyuklia lakini wakati huo huo Balozi wa Iran mjini Doha leo Jumatano amesema kuwa ziara ya Rais Raisi huko Qatar itafanyika wiki ijayo.
Viongozi wa Qatar siku kadhaa zijazo wanatazamiwa kuwa wenyeji wa mkutano mkubwa wa gesi huko Doha. Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani tarehe 27 Januari mwaka huu alimtuma Tehran Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kumkabidhi Rais Ebrahim Raisi barua ya mwaliko kwa ajili ya kushiriki katika mkutano huo mkubwa wa gesi kama mgeni maalumu.
Iran ndiyo nchi iliyo na akiba kubwa zaidi ya gesi duniani baada ya Russia; huku Qatar ikishika nafasi ya tatu kwa utaratibu. Wakati huo huo Iran na Qatar zina chanzo kikubwa zaidi cha pamoja cha gesi asilia duniani.
Algeria, Bolivia, Misri, Equatorial Guinea, Iran, Libya, Nigeria, Qatar, Russia, Trinidad na Tobago na Venezuela zinashiriki katika mkutano huo kama nchi wanachama wakuu wa Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Gesi Duniani huku Uholanzi, Norway, Iraq, Oman, Peru na Jamhuri ya Azerbaijan na Imarati zikiwa ni nchi wanachama watazamaji wa jumuiya hiyo.