Hatua isiyo ya kibinadamu ya Saudia ya kubomoa Jeddah yawakasirisha wananchi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i80570-hatua_isiyo_ya_kibinadamu_ya_saudia_ya_kubomoa_jeddah_yawakasirisha_wananchi
Manispaa ya mji wa Jeddah nchini Saudia imeendelea kubomoa nyumba za raia katika mji huo licha ya malalamiko ya wananchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 20, 2022 09:57 UTC
  • Hatua isiyo ya kibinadamu ya Saudia ya kubomoa Jeddah yawakasirisha wananchi

Manispaa ya mji wa Jeddah nchini Saudia imeendelea kubomoa nyumba za raia katika mji huo licha ya malalamiko ya wananchi.

Hatua hiyo isiyo ya kibinadamu imezusha kelele na malalamiko mengi hata katika mitandao ya kijamii.

Hadi sasa kwa akali vitongoji 10 katika mji wa Jeddah vimebomolewa na kuangamizwa kabisa na vikosi vya Manispaa ya mji huo, huku operesheni ya kubomoa nyumba za vitongoji vingine 10 ikiendelea.

Serikali ya Saudi Arabia imedai kuwa, kubomolewa nyumba katika maeneo ya makazi ya watu katika mji wa Jeddah ni sehemu ya mpango wa serikali wa kupisha miradi mikubwa.

Mpango huo unalenga takribani vitongoji 60 vya mji wa Jeddah ambavyo akthari ya nyumba zake zipo kusini mwa mji huo na inaelezwa kuwa, bomoa bomoa hiyo inatarajiwa kuendelea kwa miezi kadhaa.

Bomoa bomoa ya nyumba katika mji wa Jeddah ikiendelea licha ya malalamiko ya wananchi

 

Wanaharakati wa mitandao ya kijamii nchini Saudia wamesambaza video zinazoonyesha nyumba zikibomolewa ambapo wamelaani vikali uamuzi huo unaolenga kufuta kabisa vitongoji hivyo.

Mtandao gazeti la al-Madina umeripoti kuwa, wananchi wa mji wa Jeddah mbali na kulalamikia kubomolewa nyumba zao wamelaani utendaji wa serikali yay Riyadh.

Akthari ya wananchi waliobomolewa nyumba zao wamesema, serikali haijawapatia makazi ya muda wala kuwalipa fidia na kimsingi watu waliokuwa wakimiliki nyumba sasa wamefanywa na serikali kuwa wapangaji.