Wasiwasi wa UN kuhusu kupanuka zaidi ugaidi wa ISIS kutoka Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i80578-wasiwasi_wa_un_kuhusu_kupanuka_zaidi_ugaidi_wa_isis_kutoka_afghanistan
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake kuhusu tishio la ugaidi wa kundi la Daesh (ISIS) unaoenea kutoka Afghanistan. Antonio Guterres amesema magaidi ni hodari sana katika kutumia umbwe wa madaraka.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 21, 2022 01:10 UTC
  • Wasiwasi wa UN kuhusu kupanuka zaidi ugaidi wa ISIS kutoka Afghanistan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake kuhusu tishio la ugaidi wa kundi la Daesh (ISIS) unaoenea kutoka Afghanistan. Antonio Guterres amesema magaidi ni hodari sana katika kutumia umbwe wa madaraka.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema: "Hatari ya ugaidi kusambaa zaidi nje ya Afghanistan pamoja na kuenea kunakotisha kwa janga hilo katika baadhi ya nchi za Afrika, kunaonyesha jinsi magaidi wenye ujuzi wanavyotumia ombwe wa madaraka na kupindua serikali dhaifu." 

Kamati ya Vikwazo ya Umoja wa Mataifa hapo awali ilikuwa imesema katika ripoti yake kwamba kurejea madarakani kundi la Taliban huko Afghanistan kunazidisha wasiwasi wa Afghanistan kuwa maficho salama ya magaidi wa kimataifa. Wasiwasi wa UN kuhusu kuimarika makundi ya kigaidi huko Afghanistan na kupanuka shughuli za makundi hayo katika maeneo mengine ya dunia, unatokana na hali inayotawala sasa nchini humo. Ombwe uliojitokeza huko Afghanistan baada ya kundi la Taliban kuidhibiti tena nchi hiyo mwaka jana umeyapa makundi ya kigaidi kama al Qaida na Daesh fursa ya kuzusha tena vurugu na mauaji katika nchi hiyo na kanda hii nzima ya Asia. 

Image Caption

Katika miezi michache iliyopita ghasia na mauaji yanayofanywa na kundi la kigaidi la Daesh yameongezeka kwa kiwango kikubwa nchini Afghanistan licha ya kundi la Taliban kusisitiza kuwa litalinda usalama wa watu wa nchi hiyo; na suala hili limedhihirisha wazi udhaifu wa kundi hilo linalotawala Afghanistan. Mashambulizi mawili ya kigaidi ya mwezi Oktoba mwaka jana yaliyolenga misikiti ya Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa katika majimbo ya Kandahar na Kunduz ambayo yaliua shahidi mamia ya watu na kujeruhi wengine wengi, yaliibua ukosoaji mkubwa dhidi ya serikali ya kundi la Taliban. Baada ya mashambulizi hayo wanazuoni wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia waliitaka serikali ya Taliban kutekeleza vyema majukumu yake ya kulinda usalama wa raia wote wa Afghanistan. 

Siku chache zilizopita pia magaidi walitekeleza shambulizi la kigaidi katika mkoa wa Herat na kuua raia wasiopungua saba.

Wapiganaji wa Daesh huko Afghanistan

Kutokana na kuendelea mashambulizi hayo na harakati za kigaidi za kundi la Daesh huko Afghanistan nchi jirani zimeingiwa na wasiwasi juu ya kushadidi machafuko hayo na kuvuka mipaka ya nchi nyingine.    

Kwa mantiki hiyo, katika mikutano ya pande mbili au ya pande kadhaa za kieneo na kimataifa kuhusu Afghanistan, washiriki wamekuwa wakisisitiza ulazima wa kuundwa serikali jumuishi katika nchi hiyo, na kuitaka serikali ya Taliban kuchukua hatua haraka na ipasavyo ili kuzuia harakati za makundi ya kigaidi likiwemo kundi la Daesh nchini Afghanistan.

Kujihusisha kwa kundi la Taliban na migogoro mbalimbali nchini Afghanistan kumelifanya kundi hilo lisizingatia zaidi sera na hatua madhubuti za kukabiliana na ugaidi, jambo ambalo ni tishio kubwa kwa usalama wa ndani na kwa nchi za eneo hilo.

Kumekuwepo tetesi kwamba, kundi la Taliban linaachilia kwa makusudi hali inayoshuhudiwa hivi sasa nchini Afghanistan kama jibu la kundi hilo kwa hatua ya jamii ya kimataifa ya kukataa kutambua rasmi serikali ya kundi hilo na kwamba litapambana ipasayo na makundi kama Daesh na al Qaida pale litakapotambuliwa rasmi.

Alaa kulli hal, hali ya Afghanistan inaitia wasiwasi jamii ya kimataifa na kuna udharura wa kuchukuliwa hatua za haraka za kukabiliana na ukosefu wa amani na mashambulizi ya mara kwa mara nchini humo kabla hayajavuka mipaka na kuzikumba nchi nyingine za kanda hii.