Nabih Berri: Lebanon imepatwa na corona ya kisiasa
Spika wa Bunge la Lebanon amesema kuwa Lebanon imekumbwa na corona ya kisiasa na imezingirwa na baadhi ya nchi za Kiarabu, lakini haijawahi kufilisika.
Katika mahojiano yake na gazeti la Misri la Al-Ahram siku ya Jumapili, Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri alisema kuwa Lebanon haiwezi kuendelea kuwepo bila ya kuwa na misimamo ya wastani na umoja, na haiwezekani kupambana na Israel isipokuwa kwa umoja wa Walebanoni. Nabih Berry amesisitiza kuwa njia bora ya kupambana adui yeyote, ikiwemo Israeli, ni umoja wa ndani.
Amegusia pia uchaguzi unaotarajiwa kufanyika nchini Lebanon na kusema: Hakuna mtu anayeweza kuzuia uchaguzi huo, na kwamba taarifa alizozipata kutoka kwa marais, mawaziri na mabalozi wa nchi mbalimbali ni kwamba wanakubaliana kufanyika kwa uchaguzi wa Lebanon mwezi ujao.
Spika wa Bunge la Lebanon pia amekosoa misimamo ya baadhi ya nchi za Kiarabu dhidi ya nchi hiyo na kusema Waarabu wanaizingira Lebanon.
Wabunge wa Lebanon wametangaza kuwa uchaguzi wa Bunge wa nchi hiyo utafanyika Machi 27, mwaka huu wa 2022.
Lebanon imekuwa ikikabiliwa na maandamano makubwa tangu Oktoba 2019 kupinga hali mbaya ya maisha, maandamano ambayo yamepelekea kujiuzulu kwa Saad al-Hariri kama waziri mkuu.