Sana'a: Umoja wa Mataifa unaingiza siasa katika masuala ya kibinadamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i80644-sana'a_umoja_wa_mataifa_unaingiza_siasa_katika_masuala_ya_kibinadamu
Kaimu wa Wizara ya Haki za Binadamu ya Serikali ya Uokoaji wa Kitaifa ya Yemen amekosoa misimamo ya kindumakuwili ya Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, umoja huo unaingiza siasa katika kadhia ya kibinadamu na kuficha jinai na uhalifu unaofanywa na wavamizi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 22, 2022 08:24 UTC
  • Sana'a: Umoja wa Mataifa unaingiza siasa katika masuala ya kibinadamu

Kaimu wa Wizara ya Haki za Binadamu ya Serikali ya Uokoaji wa Kitaifa ya Yemen amekosoa misimamo ya kindumakuwili ya Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, umoja huo unaingiza siasa katika kadhia ya kibinadamu na kuficha jinai na uhalifu unaofanywa na wavamizi.

Ali al-Dailami amesema kuwa Umoja wa Mataifa, badala ya kudhamini haki za raia wa Yemen, unafunika na kuficha jinai na uhalifu unaofanywa na wavamizi na kuingiza siasa katika masuala ya kibinadamu. 

Al-Dailami ameongeza kuwa, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanafumbia macho jinai za vikosi vamizi dhidi ya raia na wakimbizi hususan nchini Yemen.

Kaimu wa Wizara ya Haki za Binadamu ya Serikali ya Uokoaji wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa, Umoja wa Mataifa unalazimika kutekeleza majukumu yake mkabala wa jinai zinazoendelea kufanywa na wavamizi, la sivyo utahesabiwa kuwa ni mshirika katika jinai na uhalifu huo.

Yemen

Ingawa mashirika ya Umoja wa Mataifa kama Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNICEF yamekuwa yakionya mara kwa mara kwamba watu wa Yemen wanakabiliwa na baa la janga na maafa makubwa ya binadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika karne moja iliyopita kutokana na  mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika kwake nchini humo, lakini hadi sasa umoja huo haujachukua hatua yoyote ya maana ya kusitisha hujuma na mashambulizi hayo. 

Maelfu ya raia wa Yemen wameuwa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na hujuma na mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake wakisaidiwa na Marekani, utawala haramu wa Israel na nchi nyingine kadhaa za Magharibi.