Jihad al Islami yailaani Israel kwa kujaribu kumuua kigaidi kiongozi wake
Harakati ya Jihadi al Islami ya Palestina imeulaani utawala wa Kizayuni kwa kujaribu kumuua kigaidi mmoja wa viongozi waandamizi wa harakati hiyo na kulitaja jaribio hilo kuwa ni jinai iliyo wazi.
Khader Adnan, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa harakti ya Jihad al Islami ya Palestina alisalimika kuuawa baada ya kushambuliwa kwa risasi juzi Jumamosi katika mji wa Nablus wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Alikuwa anazitembelea familia za mashahidi wa Kipalestina huko Nablus kabla ya genge la kigaidi la Kizayuni kumshambulia kwa risasi.
Jana Jumapili, Adnan mwenyewe alisema, ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba shirika la kijasusi la Israel MOSSAD ndilo lililomshambulia kwa risasi huko Nablus. Adnan hakupata madhara yoyote katika jinai hiyo, lakini ndugu wa kiume wa mashahidi watatu walijeruhiwa katika shambulio hilo lililofeli.
Hivi karibuni shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni MOSSAD lilitangaza kuwa litaendelea kuwaua kigaidi viongozi wa harakati za muqawama za Palestina.
Baada ya jaribio hilo, Katibu wa Jihad al Islami ya Palestina Ziyad al Nakhalah ameelezea kukasirishwa sana na jinai hiyo na kusema kuwa ni uhalifu wa wazi uliofanywa na majasusi wa Kizayuni. Amesema, Jihad al Islami inalihesabu jaribio hilo kuwa ni shambulio dhidi ya harakati hiyo nzima na halitoachwa kupita vivi hivi bila ya majibu.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS nayo imelaani vikali jaribio hilo na kulaumu pande zote zilizohusika. Tangu muongo wa 1950, utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya viongozi wa Palestina na hiyo ni katika ajenda zake kuu.