Syria yalaani propaganda za nchi za Magharibi dhidi ya Russia
Syria imelaani vikali propaganda za nchi za Magharibi, hasa Marekani dhidi ya Russia na kusema zinapotosha ukweli, zinakuza mambo kupita kiasi na zinachochea mgogoro kwa ajili ya kuendeleza satwa yao ya kibeberu duniani.
Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesema Russia ina kila haki ya kujilinda na kukabiliana na tishio na njama za nchi za Magharibi na hasa Marekani.
Taarifa hiyo aidha imesema, nchi za Magharibi, na hasa Marekani, zimekuwa zikikiuka sheria za kimataifa na zimewaua mamilioni ya watu wasio na hatia katika vita maeneo mbali mbali ya dunia kama vile Vita vya Korea, Vita vya Vietnam na pia vita katika nchi kama vile Afghansitan, Iraq na Syria. Kwa msingi huo nchi za Magharibi hazina ustahiki wa kuzungumza kuhusu sheria za kimataifa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kusimama kidete kukabiliana na sera za kibeberu za Magharibi na Marekani ambazo ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa.
Oparesheni za kijeshi za Russia nchini Ukraine zilianza Alkhamisi iliyopita kufuatia amri ya Rais Vladimir Putin wa Russia na baada ya kuwa ametambua uhuru wa maeneo ya Donbass yaliyotangaza kujitenga na Ukraine.. Putin alisema kwamba jeshi la nchi hiyo limeanzisha "operesheni maalumu ya kijeshi" hiyo kwa lengo la kuiondoa Ukraine katika hali ya kijeshi na kwamba Moscow haina nia ya kuvamia ardhi ya nchi hiyo.