Jeshi la Yemen latungua ndege ya kivita ya Saudia iliyoundwa Marekani
Jeshi la Yemen limetangaza kutungua ndege ya kivita isiyo na rubani au drone ya muungano vamizi wa Saudia Arabia iliyoundwa Marekani aina ya ScanEagle ambayo ilikuwa inaruka katika mkoa wa Hajjah kaskazini mwa Yemen.
Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema katika ukurasa wake wa Twitter Jumatatu kuwa, kikosi cha ulinzi wa anga cha jeshi hilo kimefanikiwa kutungua drone hiyo ambayo ilikuwa inatekeleza oparesheni za kivita katika wilaya ya Harad.
Jeshi la Yemen hadi sasa limefanikiwa kutungua idadi kubwa ya ndege za kivita zisizo na rubani za muungano vamizi unaoongozwa na Saudia.
Hayo yanajiri wakati ambao Jeshi la Yemen limeweza kupata mafanikio katika vita dhidi ya mamluki wanaopata himaya ya Saudi Arabia katika mkoa wenye utajiri wa mafuta wa Ma'rib ambapo limefanikiwa kudhibiti eneo la kistratijia kusini magharibi mwa mji mkuu wa mkoa huo.
Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ikishirikiana na UAE na kwa himaya ya Mareakni na utawala haramu wa Israel na madola mengine ya magharibi ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.
Vita vilivyoanzishwa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen na kuendelea hadi sasa vimeshapelekea mamia ya maelfu ya watu wasio na hatia kupoteza maisha, mbali na kuwaacha mamilioni wakiwa hawana pa kuishi. Aidha vita hivyo vimesababisha matatizo mengi ya ukosefu wa chakula, matibabu na elimu kwa watu wa Yemen.
Katika kulipiza kisasi jinai hizo, Jeshi la Yemen hutekeleza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya maeneo ya kistratijia ya Saudi Arabia na UAE.