Askari wa Israel washambulia Wapalestina katika sherehe za Isra na Mi’raj
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i80902-askari_wa_israel_washambulia_wapalestina_katika_sherehe_za_isra_na_mi’raj
Wanajeshi wa utawala haramu wa Israel wamewashambulia Wapalestina waliokuwa wamekusanyika katika mji wa Quds (Jerusalem) kwa ajili ya sherehe ya Kiislamu ya Isra na Mi’raj.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 01, 2022 07:54 UTC
  • Askari wa Israel washambulia Wapalestina katika sherehe za Isra na Mi’raj

Wanajeshi wa utawala haramu wa Israel wamewashambulia Wapalestina waliokuwa wamekusanyika katika mji wa Quds (Jerusalem) kwa ajili ya sherehe ya Kiislamu ya Isra na Mi’raj.

Kwa mujibu wa taarifa miongoni mwa waliojeruhiwa katika hujuma hiyo ya askari wa Israel ni watoto akiwemo mtoto mchanga wa miezi sita.

Hujuma hiyo ilijiri Jumatatu usiku wakati Wapalestina walipokuwa wamekusanyika katika eneo la Bab al Amoud kuadhimisha siku kuu ya Isra an Mi’raj. Katika siku hii Waislamu huadhimisha usiku ambao kulijiri safari ya kimuujiza ya  Mtume Muhammad SAW kutoka mji mtakatifu wa Makka hadi katika Msikiti wa Al Aqsa mji wa Quds na kisha baada ya hapo kwenda hadi mbinguni na kisha akarejea tena Makka usiku huo huo.

Malefu ya Waislamu wa Palestina walikusanyika katika Msikiti wa Al Aqsa kuadhimisha tukio hilo muhimu huku askari wa utawala haramu wa Israel wakitekeleza njama za kuvuruga sherehe hiyo.

Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel

Aidha jana pia askari wa utawala haramu wa Israel walishambulia kambi ya wakimbizi wa Jenin katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kumuua shahidi Mpalestina aliyetambuliwa kwa jina la Abdullah al Hasri.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesema kuwa, mapambano ya kupigania ukombozi wa Palestina yamepata nguvu na kuimarika kuliko wakati wowote ule huku adui akidhoofika kuliko kipindi chochote kile. Ziyadh al-Nakhala, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amesema hayo katika mkutano wa "Muqawama, Njia ya Ukombozi" ambapo sambamba na kuashiria vita vya Seif al-Quds amesisitiza kuwa, vita hivyo vilithibitisha kwamba, nguvu ya taifa la Palestina si yenye kwisha na imezidi kuimarika.