Mtandao mwingine mpya wa ujasusi wa Israel wasambaratishwa nchini Lebanon
Duru za habari zimeripoti kuwa, vikosi vya usalama vya Lebanon vimegundua na kuuangamiza mtandao mwingine mpya wa ujasusi nchini humo uliokuwa ukilifanyia kazi shirika la ujasusi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Mossad.
Kitengo cha intelijensia cha vikosi vya usalama wa ndani vya Lebanon leo kimefanikiwa kuusambaratisha mtandao mpya wa ujasusi wa Mossad kufuatia operesheni kiliyotekeleza katika nyumba mbili zilizoko kwenye mji wa al-Ghaaziyah na kuwatia mbaroni watu watatu wanaoshirikiana na utawala wa Kizayuni.
Taarifa za kiintelijensia zinaeleza kwamba, majasusi hao wameipatia Mossad taarifa kadhaa za hali ya ndani ya Lebanon na wamekuwa wakiwasiliana na maajenti wa shirika hilo la ujasusi la Israel kwa njia ya intaneti kwa kutumia jumbe zinazotumia alama za siri.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kwa kupatiwa taarifa hizo za ujasusi, maajenti wa Mossad walikuwa wakiwapatia vitita vya fedha majasusi wao hao wa ndani ya Lebanon kwa kutumia vifurushi maalumu ambavyo walikuwa wakivituma maeneo ya mbali yakiwemo ya majangwani.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, kwa kutumia taarifa maalumu walizokuwa wakipatiwa, vibaraka hao wa utawala wa Kizayuni waliweza kuvipata vifurushi hivyo vya fedha na kuendelea na kazi yao ya ujasusi.
Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Miqati, amepongeza na kusifu kazi iliyofanywa na vikosi vya usalama wa ndani hususan kitengo chake cha intelijensia katika kulinda usalama na kuzuia uvurugaji wa amani, kwa kusambaratisha mitandao ya kijasusi ndani ya ardhi ya nchi hiyo.../