Bin Salman anatafuta kinga ya kutofikishwa mahakamani Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81280-bin_salman_anatafuta_kinga_ya_kutofikishwa_mahakamani_marekani
Serikali ya Riyadh inatumia ongezeko la bei ya mafuta na gesi kama wenzo wa kupata kinga ya kutofikishwa mahakamani mrithi wa ufalme wa nchi hiyo, Muhammad bin Salman huko Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2022 20:33 UTC
  • Bin Salman anatafuta kinga ya kutofikishwa mahakamani Marekani

Serikali ya Riyadh inatumia ongezeko la bei ya mafuta na gesi kama wenzo wa kupata kinga ya kutofikishwa mahakamani mrithi wa ufalme wa nchi hiyo, Muhammad bin Salman huko Marekani.

Afisa mmoja wa serikali ya Saudi Arabia ameuambia mtandao wa Saudi Wikileaks kwamba maafisa wa Riyadh wanafanya mazungumzo na serikali ya Washington kwa ajili ya kutoa kinga ya kutofikishwa mahakamani Muhammad bin Salman na kwamba kumepatikana maendeleo katika uwanja huo. Afisa huyo amesema, mashauriano ya pande mbili bado yanaendelea. 

Afisa huyo wa Saudi Arabia amesema mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo anafanya jitihada za kutumia mgogoro wa Ukraine na kupanda juu kwa bei ya mafuta kwa maslahi yake binafsi hususan kuzidisha nafasi yake nchini Marekani; ikiwa ni pamoja na kutupiliwa mbali kesi zinazomkabili katika mahakama za Marekani kama ile ya mauaji ya mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudia, Jamal Khashoggi na jaribio la kutaka kumuua Saad al Jabri. 

Saad al Jabri ambaye alikuwa mshauri wa mrithi wa zamani wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Nayef, amewasilisha mashtaka mahakamani dhidi ya Muhammad bin Salman na maafisa wengine kadhaa wa serikali ya kifalme ya Saudi Arabia wakiwemo wasaidizi wakuu wa Bin Salman, Saud al Qahtani, Ahmed al Asiri na Badr al Asaker kwa tuhuma za kutaka kumuua kwa njia kama ile iliyotumiwa kumuua mwandishi na mkosoaji wa utawala wa Riyadh, Jamal Khashoggi.

Mashtaka hayo pia yamesisitiza kuwa Idara ya Upelelezi ya Marekani imezima jaribio la kutaka kumuua al Jabri nchini Canada baada ya kuwasiliana na serikali ya nchi hiyo.

Saad al-Jabri

Saad al-Jabri, ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Canada na anayejulikana kama "Kisanduku Cheusi cha Aal Saud", ana nyaraka muhimu zinazomhusu mfalme Salman bin Abdul-Aziz pamoja na mwanawe, Muhammad bin Salman ambaye ni mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo ambapo kama nyaraka hizo zitavuja na kusambazwa zinaweza kuharibu mno haiba ya bin Salman ulimwenguni.

Mwanamfalme wa Saudi Arabia na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo, Muhamamd Bin Salman amekuwa akitumia mbinu ya mauaji kuwamaliza wapinzani wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo.