Mar 15, 2022 10:54 UTC
  • Unyongaji wa umati; jinai maalumu ya ukoo wa Aal Saud

Ikiwa ni katika kuendeleza jinai dhidi ya watu wa Saudi Arabia, utawala wa nchi hiyo umechukua hatua isiyo ya kawaida ya kunyonga kwa umati watu 81 katika siku moja.

Kuna nukta saba muhimu zinazopasa kuzingatiwa katika hatua hiyo ya kijinai iliyotekelezwa na utawala wa Saudia.

Nukta ya kwanza ni kuwa hatua hiyo ni jinai dhidi ya binadamu. Kifungu cha 7 cha Hati ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kinafafanua uhalifu dhidi ya binadamu kuwa ni vitendo maalumu vya kimfumo au vilivyoenea dhidi ya raia wa kawaida. Utawala wa Aal-Saud umewakata vichwa raia 81 wa Saudia katika siku moja. Kwa kufanya hivyo, Wasaudi wamewapokonya haki ya kuishi makumi ya raia wa Saudia, wakati haki ya kuishi kwa mujibu wa sheri za kimataifa ni moja ya haki zisizopaswa kukiukwa au kubatilishwa.

Nukta ya pili ni kuwa miongoni mwa walionyongwa ni vijana 41 wa Kishia wa eneo la Qatif nchini Saudia ambao awali walikamatwa na kufungwa jela na utawala wa Saudia kwa visingizio mbalimbali. Kuwepo idadi hiyo ya vijana wa Kishia miongoni mwa walionyongwa kunaonyesha kuwa, utawala huo kwa mara nyingine tena umefanya jinai kubwa kwa msingi wa mitazamo ya kiidiolojia na kiitikadi. Utawala wa Saudia kimsingi unawaadhibu kinyama wale wanaoupinga au kukosoa sera zake, na hata kuwanyima haki ya kuishi kwa kuwanyonga.

Mazishi ya wahanga wa jinai ya kunyongwa kwa umati Saudia

Kuhusu kadhia hiyo, Kazem Gharibabadi, Katibu wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Iran anasema: "Katika orodha ya walionyongwa, huenda kuna watu ambao walihukumiwa kwa mtazamo wa mahakama ya Saudia, lakini la muhimu ni kuwa niliona kwenye vyombo vya habari katika mgawanyo wa wale waliouawa, jambo lililonifanya niamini kuwa suala lililopelekea wanyongwe ni mitazamo yao ya kiidiolojia na kiitikadi, suala ambalo ni hatari kubwa."

Nukta ya tatu: Suala jingine ni kwamba utawala wa Saudia umewanyonga raia wake kwa misingi isiyokuwa na uwazi. Kwa hakika utawala huo umewanyonga watu wasio na hatia kwa msingi wa mashtaka na tuhuma za uwongo na zisizothibitishwa kisheria. Hamza al-Shakhouri, mmoja wa maafisa wa ngazi za juu  wa Jumuiya ya Upinzani katika Bara Arabu anasema: "Watawala wa Saudia hawaweki wazi msababa mauaji hayo na wala wanachosema si cha kuaminika. Hukumu za kifo nchini Saudi Arabia hazitokani na shutuma za wazi, lakini zinatokana na tuhuma bandia na za uongo."

Nukta ya nne muhimu ni kwamba watu walionyongwa hawakufanyiwa uadilifu kupitia mkondo wa haki wa uendeshaji kesi ya haki, bali kama zilivyokuwa tuhuma bandia walizoelekezewa mashtaka dhidi yao pia yaliendeshwa kwa msingi wa uzushi na uongo. Katika uwanja huo, watumiaji wa mitandao ya kijamii wa Saudia na hasa wa twitter wamechukizwa na jinai hiyo ya watawala wa Aal Saud dhidi ya raia 81 wa Saudia, wengi wao wakiwa Mashiana na kuandika: "Kilichotokea ni mauaji ya umati dhidi ya watu wasio na hatia na ambao wamehukumiwa bila viwango vya chini zaidi vya haki na uadilifu kuzingatiwa. Kazem Gharibabadi pia ameandika:  "Jambo la kwanza kuhusu mauaji ya Jumamosi nchini Saudi Arabia ni jinsi mahakama ilivyoendesha mashtaka na vipi watu 81 wanaweza kunyongwa katika siku moja."

Nukta ya tano muhimu ni kwamba wafungwa wawili wa kivita wa Yemen ni miongoni mwa walionyongwa. Hata hivyo, kulingana na vyombo mbalimbali vya sheria za kimataifa, kuheshimu utu wa wafungwa wa vita ni mojawapo ya majukumu ya serikali. Kwa mujibu wa serikali ya Yemen, wafungwa wawili wa kivita wa Yemen waliofungwa nchini Saudi Arabia ni miongoni mwa watu 81 walionyongwa na utawala wa Saudia kinyume cha sheria za kimataifa.

Watuhumiwa wakinyongwa hadharani Saudia

Nukta ya sita: Utumiaji mabavu, jinai na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ndani ya Saudi Arabia umeongezeka kwa kasi kubwa tangu Mohammed bin Salman aingie madarakani na taratibu kuchukua nafasi ya mtawala mkuu wa nchi hiyo ya kifalme. Kutiwa mbaroni kwa wanawafalme kwa kisingizio cha kupambana na ufisadi, kukamatwa na kupewa vifungo vya muda mrefu jela kwa mashekhe na wanaharakati wa kiraia, pamoja na mauaji ya kikatili ya mwandishi wa habari wa Saudia Jamal Khashoggi huko Istanbul Uturuki, ni baadhi tu ya jinai hizo. Ikilaani kunyongwa watu 81 kwa siku moja, tovuti ya habari ya Harakati ya Mabadiliko na Uhuru ya Saudi imeandika: "Tangu Muhammad bin Salman aingie madarakani Juni 2017, amewapa ishara ya taa ya kijani kibichi vibaraka wa utawala wake kukabiliana, kuua na kuwanyonga wapinzani wake wa kisiasa."

Nukta ya saba ni kuwa jambo linalotia uchungu mkubwa zaidi hata kuliko kunyongwa huko kwa raia 81 kwa siku moja, ni kimya cha nchi za Magharibi mbele ya jinai hiyo ya kushtua. Ukimya huo unathibitisha kwa mara nyingine kwamba mwelekeo wa nchi za Magharibi kuhusu suala zima la haki za binadamu ni wa kundumakuwili. Pale ambapo maslahi yao na ya washirika wao yanapokuwa hatarini, huamua kupiga makelele na kutumia vibaya suala zima la haki za binadamu lakini pale maslahi yao au ya washirika wao yanapokuwa hayako hatarini, hunyamazia kimya suala hilo na kulifanya lisiwe na maana kabisa.

Tags