Asaeb Ahlul Haq Iraq: Ikiwa uvamizi wa Marekani utaendelea, silaha za muqawama zitatoa jibu
Harakati ya Asaeb Ahlul Haq nchini Iraq imetangaza kuwa itaanzisha mapambano ya silaha iwapo Marekani haitaondoka katika ardhi ya Iraq hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya wajumbe wa Uratibu wa Makundi ya Kisiasa ya Iraq kukutana na kiongozi wa mrengo wa Sadr Alkhamisi iliyopita ili kujadili hatua za kivitendo za kupambana na ufisadi, kuwafungulia mashtaka wafisadi, kukomesha ubadhirifu wa kimakusudi wa mali ya umma, na kuyafukuza majeshi ya kigeni katika ardhi ya Iraq kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa. Makundi hayo pia yalijadili suala la kuhakikisha silaha zote zinakabidhiwa kwa serikali na kulindwa harakati ya al-Hashdul al-Shaabi, kwa njia ambayo inaimarisha nafasi yake katika kudumisha usalama wa Iraq.
Ahmad Abdul Hussein mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Asaeb Ahlul Haq nchini Iraq amesema katika mahojiano yake na "Al-Ahd" kuwa iwapo wanajeshi wa Marekani hawataondoka Iraq kufikia mwisho wa mwaka huu, wanamuqawama watakabiliana kwa silaha na vamizi wa Marekani.
Amesisitiza kuwa: “Iwapo majeshi ya Marekani hayataondoka Iraq ifikapo tarehe 31 Disemba, silaha za muqawama zitakuwa tayari kujibu." Abdul Hussein amesema: "Silaha za wanamuqawama zitaendelea kuwepo mikononi hadi mwanajeshi wa mwisho wa Marekani atakapoondoka Iraqi kwa wakati ulioainishwa." Ameongeza kuwa, katika mkutano wao na kiongozi wa vuguvugu la Sadr, kulifikiwa makubaliano kuhusu ulazima wa kuondolewa majeshi yote ya kigeni kwa ujumla nchini Iraq, hususan majeshi ya Marekani na kulindwa uhuru wa Iraq.

Tarehe 26 Julai mwaka jana, Baghdad na Washington zilikubali kuondoa wanajeshi wa kivita wa Marekani nchini Iraq ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, na kuacha idadi ndogo tu ya wanajeshi wa Marekani kwa ajili ya kutoa ushauri na mafunzo kwa vikosi vya jeshi la Iraq.
Tarehe 5 Januari mwaka 2020 Bunge la Iraq lilipasisha azimio la kufukuzwa vikosi vya majeshi ya nchi za kigeni hususan Marekani katika ardhi ya Iraq. Uamuzi huo wa Bunge la Iraq ulichukuliwa baada ya jeshi la Marekani kufanya mauaji ya kigaidi dhidi ya Luteni Jenerali Qassim Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Abu Mahdi al-Muhandis aliyekuwa afisa wa wapiganaji wa kujitolea wa harakati ya al Hashdul Shaabi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad.
Kufuatia jinai hiyo iliyofanywa na ndege za kivita za Marekani kwa amri ya moja kwa moja ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump, mnamo Januari 8 mwaka 2020, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilichukua hatua ya kulipiza kisasi kwa kuvurumisha makombora kadhaa dhidi ya kambi ya wanajeshi wa Marekani ya Ain al Assad nchin Iraq na kuisawazisha kabisa na ardhi.