Spika wa Lebanon: Iran ndio chimbuko kuu la muqawama katika eneo
Spika wa Bunge la Lebanon ameitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama chanzo kikuu cha harakati za muqawama katika eneo la Asia Magharibi, zilizoipa ilhamu kambi ya muqawama kote duniani.
Nabih Berri alisema hayo jana Alkhamisi katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hosseini Amir-Abdollahian ambaye yuko Beirut kwa ziara rasmi ya kikazi.
Berri ameeleza bayana kuwa, kitendo cha baadhi ya madola ya Kiarabu cha kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kuipa mgongo kadhia muhimu ya Palestina.
Spika wa Bunge la Lebanon ameashiria uhaba wa mafuta katika nchi yake na kueleza kuwa, Iran ilitekeleza ahadi yake na kuipa mafuta nchi hiyo ya Kiarabu, na kuonesha mshikamano na taifa hilo katika kipindi kigumu cha matatizo ya petroli.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amir-Abdollahian amesema Tehran ipo tayari kushirikiana na Lebanon katika uga wa nishati, na kuikidhia mahitaji yake ya umeme na gesi.
Amesema Iran ipo tayari kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na kibiashara na taifa jirani na rafiki la Lebanon, na kushirikiana kwenye mambo yenye maslahi ya pamoja.
Aidha jana Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikutana na kufanya mazungumzo na Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon, na vilevile Waziri Mkuu wa nchi hiyo Najib Miqati.