Aug 12, 2022 07:40 UTC
  • Israel imewaua shahidi watoto Wapalestina zaidi ya 1,000 tangu 2008

Tangu mwaka 2008, zaidi ya watoto elfu moja wa Kipalestina wameuawa shahidi katika Ukanda wa Gaza katika mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel

Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya Al-Mayadeen siku ya Alkhamisi, mashahidi 15 kati ya 43 wa mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza walikuwa watoto, na takwimu rasmi sasa zinaonyesha kuwa jumla ya watoto wa Kipalestina waliouawa shahidi na Israel tangu mwaka 2008 imefikia zaidi ya elfu moja.

Kwa mujibu wa ripoti hii, watoto na vijana ni asilimia 47 ya wakazi wa Ukanda wa Gaza, na watoto wanne kati ya watano wanakabiliwa na matatizo ya kiakili, ikiwa ni pamoja na huzuni, wasiwasi na hofu iliyosababishwa na hujuma za utawala dhalimu wa Israel.

Kwa mujibu wa ripoti hii, watoto watatu kati ya watano wa Kipalestina wanajaribu kujidhuru kutokana na matatizo ya akili.

Utawala wa Israel unaokalia Quds Tukufu kwa mabavu umekuwa ukiuzingira Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya miaka 15, na kizazi kizima cha watoto wa Kipalestina kimeishi chini ya kivuli cha mzingiro huo wa kinyama.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesisitiza kuwa mzingiro wa  Gaza ni sehemu ya jinai za kibaguzi zinazofanywa na wakaaji wa Jerusalem.

Jinai ya Israel katika maeneo ya raia katika Ukanda wa Gaza

Tangu mwaka 2008 utawala wa Israel umeanzisha vita vinne katika ardhi ya Palestina na kuua karibu watu 4,000 ambao robo yao ni watoto.

Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amebainisha wasiwasi wake juu ya kiwango ambacho utawala wa Israel umekuwa ukiwaua watoto wa Kipalestina hadi sasa mwaka huu.

Akizungumza Alhamisi, Michelle Bachelet  amesema, "Kumdhuru mtoto yeyote wakati wa mzozo kunasumbua sana, na mauaji na ulemavu wa watoto wengi mwaka huu ni jambo lisilokubalikka."

Hadi sasa mwaka huu, watoto 37 wa Kipalestina wameuawa mikononi mwa wanajeshi katili wa Israel. Idadi hiyo inajumuisha watoto ambao waliuawa shahidi kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa Israel ya mfululizo dhidi ya  Ukanda wa Gaza.

Aidha amesema sheria ya kimataifa ya kibinadamu iko wazi, kuanzisha shambulio ambalo linaweza kutarajiwa kuua au kuumiza raia, au kuharibu vitu vya kiraia ni marufuku na amesema mashambulizi hayo ya Israel dhidi ya Wapalestina lazima yakomeshwe.

Tags