Oct 02, 2022 02:14 UTC
  • Sanad yalaani kuongezeka hukumu za kikatili nchini Saudi Arabia

Shirika la kutetea haki za binadamu la "Sanad" limetangaza kuwa kumeshuhudiwa ongezeko la kukamatwa wakosoaji na hukumu za kikatili na kidhalimu nchini Saudi Arabia katika kipindi cha hivi karibuni.

Saudi Arabia hususan baada ya kuteuliwa Mohammed bin Salman kuwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme, imechukua hatua kali dhidi ya waandishi na wanaharakati wa masuala ya kiraia na imewatia mbaroni makumi ya maulama, wana wafalme, waandishi, washairi na wanaharakati wa kidini kwa kisingizio cha kutishia usalama wa nchi hiyo na kuwahukumu baadhi yao vifungo na kunyongwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Saudi Leaks, shirika la kutetea haki za binadamu "Sanad", limetangaza kuwa utawala wa Saudia unaendelea kuwashikilia wanaharakati sambamba na kutimia mwaka wa tano wa wimbi la kamatakamata ya kidhalimu iliyoanza Septemba 2017, ambayo ililenga kundi la walinganiaji wa Kiislamu na wanaharakati.

Shirika la Haki za Kibinadamu la Sanad limeongeza kuwa, Malik Al-Darwish ambaye aliachiwa huru chini ya mwezi mmoja uliopita kutoka jela za Saudia, amekamatwa tena na vyombo vya usalama vya nchi hiyo.

Limeongeza kuwa, mwanaharakati Sami Al-Amiri, mkazi wa Makka, pia amekamatwa kwa sababu tu ya kuandika shairi ambalo limezungumzia suala la Palestina na baadhi ya matukio ya kisiasa.

Saudi Arabia

Shirika la kutetea haki za binadamu la Sanad limetoa wito wa kuheshimiwa uhuru, sheria na kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa katika korokoro za Saudia bila ya hatia yoyote.

Vilevile majaji 10 waliokamatwa Aprili 2022 wamehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.

Duru za kisheria zimelaani hukumu hizo na kutoa wito wa kuzidishwa mashinikizo kwa utawala wa Saudia ili ukomeshe kesi dhidi ya watu wasio na hatia na kuwaachia huru.

Tags