Dec 06, 2022 02:17 UTC
  • Wapalestina 160 wameuawa shahidi tangu kuanza mwaka huu

Kwa akali Wapalestina 160 wameuawa shahidi na jeshi la utawala haramu wa Israel katika ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan tangu kuanza mwaka huu wa 2022.

Sambamba na mauaji hayo, wanajeshi wa Israel wakishirikiana na walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakifanya hujuma katika maeneo mbalimbali ya Wapalestina kwa ajili ya kusukuma mbele mpango mchafu wa kujitanua Israel.

Mamia ya Wapalestina pia wamejeruhiwa katika hujuma na mashambulio ya jeshi la Israel katika maeneo mbalimbali ya Palestina tangua kuanza mwaka huu.

Ripoti kutoka Palestina zinasema kuwa, takwimu hizo hazijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Umoja wa Mataifa umetangaza katika ripoti yake kwamba mwaka huu wa 2022 unaoelekea ukingoni ulikuwa mwaka wa umwagaji damu zaidi katika ardhi za Palestina katika kipindi cha miaka 16 iliyopita.

 

Wakati huo huo jeshi la utawala haramu wa Israel limewauwa shahidi watoto 46 wa Kiipalestina tangu hadi kufikia mwezi Oktoba mwaka huu.

Tangu mwaka 2008 utawala wa Israel umeanzisha vita vinne katika ardhi ya Palestina na kuua karibu watu 4,000 ambao robo yao ni watoto wadogo.

Mapigano yanayotokea baina ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni husababisha vifo vya watu wengi wasio na hatia hasa wanawake na watoto wadogo. Watoto wa Kipalestina wanauliwa shahidi hata kama hawashiriki kivyovyote vile katika mapigano hayo. 

Tags