Hamas yaipongeza Oman kwa msimamo wake wa kususiwa utawala wa Kizayuni
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesifu na kupongeza msimamo wa Bunge la Oman katika fremu ya kushadidisha kususiwa utawala haramu wa Israel.
Taarifa ya Chama cha Hamas imesisitiza kuwa, msimamo wa Oman unabainisha na kuweka wazi msimamo asili na wa kihistoria wa nchi hiyo katika kuliunga mkono taifa la Palestina.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeyataka Mabunge yote ya Kiarabu na Kiislamu kuchukua hatua kama ya Oman ya kupasisha sheria inayotambua kuwa ni kosa na uhalifu kushirikiana na utawala dhalimu wa Israel.
Majuzi Baraza la Ushauri la Oman liliikabidhi Kamati wa Kutunga Sheria na Kulinda Haki ya nchi hiyo, muswada wa marekebisho ya kifungu cha 10 cha sheria ya kuharamisha na kupiga marufuku kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel ili upasishwe rasmi. Hatua hiyo ya Bunge la Oman, ni katika kukamilisha Dikrii ya Kifalme nambari 9/72 ya Oman kuhusu kuususia utawala wa Kizayuni na ambayo ilitolewa na Sultan Qaboos.
Dikrii hiyo ya Kifalme inatilia mkazo marufuku ya kuweka mikataba ya aina yoyote ile ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja baina ya taasisi na watu wa Oman na utawala wa Kizayuni wa Israel. Dikrii hiyo imepiga marufuku pia miamala na ushirikiano na mashirika yote ambayo yana manufaa au matawi yao katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel.
Hatua ya Baraza la Taifa la Ushauri la Oman inaonesha kuwa, uhusiano wa nchi hiyo na utawala pandikizi unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu, hauendi kwa mujibu wa matakwa ya Israel.