Jun 16, 2016 15:30 UTC
  • Maulamaa wa Bahrain: Kuipiga marufuku Al-Wifaq ni kutangaza vita

Maulamaa wa Bahrain wametangaza kuwa hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kuzifuta na kuzipiga marufuku jumuiya na asasi za upinzani, kufunga ofisi zao na kuwatia nguvuni watu ni sawa na "kutangaza vita".

Kupitia taarifa maalumu waliyotoa, maulamaa wa Bahrain wamelaani hatua kandamizi za utawala wa Aal Khalifa dhidi ya wananchi na asasi za kidini na za kisiasa za upinzani nchini humo.

Taarifa hiyo ya maulamaa wa Bahrain imezielezea sera za utawala wa Aal Khalifa kuwa ni za "kigaidi" na kuongeza kuwa uzidishaji huo mashinikizo wa kimajununi haumaanishi kitu kingine zaidi ya utovu wa mantiki na kuacha kutumia siasa na kuchagua muelekeo wa kuzusha mifarakano ya kimadhehebu dhidi ya wananchi wanaopigania haki zao za kisheria kwa njia ya amani.

Maulamaa wa Bahrain wamesisitiza kwamba utawala wa Aal Khalifa unakosea kama unadhani utaweza kuzima harakati za wananchi kwa njia ya ukandamizaji.

Taarifa ya maulamaa hao imebainisha pia kwamba harakati ya "Attau'iyatul Islamiyyah" ni anuani ya mwamko asili na uhuru wa Kiislamu nchini Bahrain; na utawala wa Aal Khalifa hauwezi kuivunja harakati hiyo kama ulivyofanya kuhusiana na Baraza la Kiislamu la Maulamaa wa Bahrain.

Mapema wiki hii ofisi zote za harakati kuu ya upinzani nchini Bahrain ya Al-Wifaq zilifungwa sambamba na kupigwa marufuku harakati nyengine mbili za upinzani za Attau'iyatul Islamiyyah na Al-Risaalah.../

Tags