Wairaqi zaidi ya milioni moja wametoweka na hawajulikani waliko
Apr 05, 2023 11:25 UTC
Umoja wa Mataifa umetangaza katika ripoti yake kuwa, zaidi ya watu milioni moja wametoweka nchini Iraq na hawajulikani waliko; katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, ikiwa ni pamoja na enzi za udikteta wa Saddam Hussein, za uvamizi wa Iraq ulioongozwa na Marekani, na za kuibuka kwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS).
Kamati ya Umoja wa Mataifa ya kuchunguza wanaotoweka kwa kulazimishwa, imechapisha ripoti ya kutoweka zaidi ya watu milioni moja katika nusu karne iliyopita nchini Iraq na kuitaka serikali ya nchi hiyo iwatafute wahanga na kuwaadhibu wasababishaji wa hali hiyo.
Aidha, kamati hiyo ya UN imeitaka Iraq ichukue hatua haraka za kubuni njia za kuzuia, kutokomeza na kufidia uhalifu huo wa kutisha.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, kati ya mwaka 1968 na 2003, zaidi ya watu 290,000 wakiwemo raia wapatao 100,000 wa Kikurdi walitoweka kwa nguvu kupitia "kampeni ya mauaji ya kimbari" iliyoendeshwa na utawala wa Saddam Hussein katika eneo la Kurdistan.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kutoweka Wairaq kuliendelea baada ya uvamizi wa Marekani wa mwaka 2003, ambao uliandamana na kukamatwa Wairaq wasiopungua 200,000, karibu nusu yao wakiwa ni wale waliokuwa wakishikiliwa katika jela za Marekani au Uingereza nchini Iraq.
Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Iraq iunde kikosi kazi huru ili upatikane uhakika kama mateka wa vita wameorodheshwa na familia zao zifahamishwe hali zao na mahali waliko.
Miaka 20 iliyopita, mnamo mwezi Machi 2003, aliyekuwa rais wa Marekani George W. Bush alitoa amri ya kushambuliwa na kuvamiwa kijeshi Iraq bila ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika hatua ya upande mmoja na kinyume cha sheria aliyochukua kwa kushirikiana na Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo Tony Blair.
Vikosi vya Marekani na Uingereza vilianzisha vita vikubwa vilivyopelekea kuanguka utawala wa Baath na kupinduliwa Saddam Hussein.../
Tags