Familia: Israel inazuia miili ya Wapalestina wanaowaua
(last modified Thu, 23 Jun 2016 08:03:55 GMT )
Jun 23, 2016 08:03 UTC
  • Familia: Israel inazuia miili ya Wapalestina wanaowaua

Familia za Wapalestina waliouawa shahidi na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamefanya maandamano kuutaka utawala wa Tel Aviv kuwapa miili ya wapendwa wao huku wakitaja sera hiyo ya kuzuia miili kuwa 'jinai na mateso kwa walio hai na waliokufa'.

Huku wakiwa wamebeba mabango yenye picha za wapendwa wao waliouawa, familia hizo zimepiga nara ya kuulani kitendo hicho cha utawala huo ghasibu, katika maandamano yaliyofanyika nje ya Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kiimabara ya Abu Kabir, katika mji wa bandari wa Jaffa. Aidha wabunge kadhaa wa Kiarabu wa bunge la utawala haramu wa Israel KNESSET walishiriki maandamano hayo ya jana Jumatano.

Utawala khabithi wa Kizayuni umeshadidisha jinai zake hizo kwa lengo la kuwapigisha magoti Wapalestina ili wasalimu amri na kughairi kuendeleza muqawama wao dhidi ya Uzayuni. Tangu mwishoni mwa mwaka jana, wakati ilipoanza Intifadha ya Quds hadi sasa, zaidi ya Wapalestija 215 wameshauliwa shahidi na maelfu ya wengine kujeruhiwa au kutiwa nguvuni. Kadhalika wasichana na wanawake 215 wameshatiwa mbaroni na wanajeshi wa Israel tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba mwaka jana.