Jun 24, 2016 14:36 UTC
  • Jumuiya za Kiislamu zalaani kuvuliwa uraia Sheikh Qassim

Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu imelaani hatua ya utawala wa Aal-Khalifa kumvua uraia mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu nchini Bahrain Ayatullah Sheikh Isa Qassim.

Ayatullah Mohsen Araki, Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo amesema vitendo visivyo vya kiadilifu kama hivyo vya utawala wa Aal-Khalifa vitawatumbukia nyongo karibuni hivi na kwamba katu haviwezi kufanikisha malengo potofu ya utawala huo. Amesema Sheikh Qassim anatoka katika kizazi kitukufu, mwenye asili na mizizi Bahrain na kwamba kizazi cha Aal-Khalifa ndio wageni kwa kuwa ndio walioanzisha hujuma ya kijeshi katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi na kunyakua ardhi zake zaidi ya karne moja iliyopita.

Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni baadhi ya nchi na asasi za kimataifa zilizotoa taarifa ya kulaani kupokonywa uraia Ayatullah Qassim.

Kadhalika maelfu ya wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano kwenye miji tofauti ya nchi hiyo na kulaani kitendo hicho walichokitaja kuwa kisicho cha kibinadamu cha utawala wa kifalme wa Aal-Khalifa cha kumvua uraia Sheikh Isa Qassim. Ikumbukwe kuwa, tarehe 20 mwezi huu wa Juni, utawala wa Manana ulichukua hatua iliyo kinyume na sheria na ubinadamu ya kumvua uraia Sheikh Isa Qassim, mwanachuo mkubwa wa nchi hiyo kwa madai kuwa ametumia vibaya nafasi yake kwa maslahi ya madola ya kigeni.

Tags