Vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya viongozi kadhaa wa Taliban
Baraza la Ulaya tarehe 20 mwezi huu wa Julai lilitangaza kuwawekea vikwazo Abdul Hakim Haqani Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Afghanistan, Abdul Hakim Sharei Waziri wa Sheria na Moulavi Habibullah Agha Kaimu Waziri wa Elimu katika serikali ya mpito ya Afghanistan kwa kuhusika katika kuwanyima wasichana na wanawake wa Afghanistan haki yao ya kupata elimu, kupata haki ya kisheria, na haki sawa na wanaume wa nchi hiyo.
Katika kujibu hatua hii ya Baraza la Ulaya dhidi yake kundi la Taliban limesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa katika fremu ya mashinikizo ya Ulaya dhidi ya Afghanistan ambayo si kwa maslahi ya upande wowote ule. Hii ina maana kuwa hatua kama hizi hazina athari katika kubadili uamuzi, mienendo na utendaji wa Taliban kuhusu masuala ya wanawake. Hii ni kwa sababu Taliban imesisitiza mara kadhaa kwamba suala la wanawake ni suala la ndani ya Afghanistan na kuzitaka nchi mbalimbali zijiepushe kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo Marekani imetangaza kuwa kundi la Taliban linapasa kuheshimu haki za kiraia za wasichana na wanawake wa Afghanistan kama sharti la kutambuliwa serikali hiyo kimataifa. Uamuzi wa Taliban wa kupiga marufuku elimu ya wasichana huko Afghanistan pia unakinzana na kanuni za kimataifa.

Asadollah Zarei mchambuzi wa masuala ya Afghanistan anazungumzia hili akisema:" Hakuna shaka kuwa masuala yanayotokea ndani ya mipaka ya Afghanistan ni masuala ya ndani, hata hivyo kutilia maanani suala la kuheshimu haki za raia hii leo limebadilishwa na kuwa kadhia ya kimataifa ambayo hata nchi za Kiislamu na maulamaa wa Kiislamu wanapambana kutetea haki hii; ambapo wanaitaka Taliban iheshimu haki za wanawake na wasichana na hasa kuhusu suala la elimu. Hii ni kwa sababu jamii ya Kiafghani pia haijaafiki uamuzi huu wa Taliban huku duru na shakhsia mbalimbali wa ndani pia wakiitaka serikali ya Taliban izingatie haki hii ya kupata elimu wasichana wa nchi hiyo.
Wakati huo huo ingawa inawezekana baadhi ya duru zikawa na malengo yake nyuma ya pazia na kutaka kunufaika na mpango huu tajwa lakini nukta muhimu ni kuwa elimu kwa wasichana si tu kuwa haijakatazwa katika mafundisho yoyote ya Kiislamu bali imesisitizwa pia katika dini. Uamuzi huu wa Taliban wa kupiga marufuku wasichana kusoma unakinzana na kanuni za kimataifa; na hii ni sababu tosha kwa duru mbalimbali kuzidisha mashinikizo dhidi ya Afghanistan.

Aref Akram mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: Haki ya kuendelea na elimu kwa wasichana ni haki iliyokubaliwa katika ngazi za kimataifa hata hivyo Taliban imekusudia kuwatwisha wananchi wa Afghanistan matakwa yake; hatua iliyokabiliwa na radiamali mbalimbali za nchi na duru mbalimbali kimataifa. Wananchi wa Afghanistan kwa zaidi ya miongo minne sasa wanataabika na matatizo mbalimbali ambayo ni natija ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, uvamizi na kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo, na ni wazi kuwa jamii ya Waafghani haiwezi tena kustahimili matatizo haya tajwa.
Ala kul haal tunaweza kusema kuwa hatua ya Baraza la Ulaya ya kuwawekea vikwazo viongozi watatu wa serikali ya Taliban kwa kukiuka haki za wanawake na wasichana ni hatua ya kwanza ya kivitendo kuwahi kuchukuliwa na nchi za Ulaya dhidi ya Taliban, hata hivyo tunaweza kutaja hapa kuwa vikwazo vya Baraza la Ulaya dhidi ya Taliban ni hatua ya kisiasa tu kwa kuzingatia kuwa dhaifu sana mahusiano ya kimataifa na safari za shakhsia waliowekewa vikwazo wa Taliban nje ya nchi au kwa uchache katika nchi za Ulaya. Ndio maana Taliban pia haikuoonyesha kukasirishwa sana na hatua hii ya Baraza la Ulaya. Ingawa Taliban hivi karibuni ilitangaza masuala kama muhtawa wa vitabu ya kufundishia kuwa ni sababu ya kupigwa marufuku elimu kwa wasichana juu ya daraja la sita lakini hakuna maelezo au ishara inayoonyesha kuanza Taliban kutoa elimu kwa wasichana huko Afghanistan; jambo lililosababisha athari haribifu za kiakili na kimwili kwa jamii ya wasichana wa Kiafghani wanaohitaji kuzingatiwa pakubwa na serikali ya Taliban. Mbali na hili, jamii ya Kiafghani inahitaji huduma ya wasichana na wanawake katika sekta na njanja mbalimbali ikiwemo sekta ya tiba ambapo kuna ulazima na umuhimu kwa wasichana kuendelea na masomo na kupata ujuzi mbalimbali wa kielimu na wa vitendo ili kuihudumia jamii ya Afghanistan.