Sep 24, 2023 02:20 UTC
  • Josep Borrell
    Josep Borrell

Josep Borrell Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya ametahadharisha kuwa umoja huo unakabiliwa na mgawanyiko mkubwa kuhusu sera za uhamiaji na kwamba suala hilo linaweza kuufanya Umoja wa Ulaya uvunjike.

Borrell amesisitiza ulazima wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kutekeleza siasa za pamoja kuhusu uhamiaji, ambapo hadi sasa nchi wanachama wa Umoja huo hazijafikia muafaka kuhusu suala la uhamiaji. Ameongeza kuwa licha ya kuanzisha mpaka wa pamoja wa nje, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinahitilafiana juu ya namna ya kusimamia ipasavyo masuala ya uhamiaji na wahamiaji. 

Josep Borrell

Sisitizo la Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya juu ya uwezekano wa kusambaratika na kuvunjika umoja huo linapata nguvu zaidi kwa kuzingatia hitilafu kubwa zinazoendelea ndani ya taasisi hiyo ya kikanda ya Ulaya kuhusu kadhia mbalimbali hasa jinsi ya kushughulikia suala la wahajiri. Ingawa mgawanyiko ndani ya Umoja wa Ulaya haukomei katika suala la uhamiaji, hasa wahamiaji haramu na wakimbizi, ambalo limetajwa kuwa changamoto kubwa zaidi ya Umoja wa Ulaya tangu kuanzishwa kwake, hata hivyo, kutokana na ukali wa suala la wakimbizi na athari zake kubwa, mzozo wa jinsi ya kukabiliana na kutatua mgogoro huu unaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya Umoja wa Ulaya na hatimaye kuusambaratisha. Suala hilo linakuwa zito sana hasa kwa nchi ndogo za Ulaya Mashariki na Kati ambazo haziko tayari kufuata maamuzi ya Umoja wa Ulaya kwa sababu ya idadi ndogo ya watu wao na mshikamano wa kitamaduni na kikabila. Kulingana na Borrell, wakati baadhi ya nchi wanachama wa EU, kama vile Uhispania, zina historia ndefu ya kukaribisha na kuwajumuisha wahamiaji katika jamii zao, nchi zingine zinapinga suala hili.

Kwa kuzingatia kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinatakiwa kutekeleza maamuzi ya Brussels, suala la uhamiaji, kivitendo, limekuwa changamoto kubwa kwa baadhi ya nchi wanachama wa umoja huo. Nchi hizi zinakabiliwa na tatizo la mgongano kati ya uhuru na maslahi ya kitaifa kwa upande mmoja, na utekelezaji wa maamuzi na sheria za Umoja wa Ulaya kwa upande mwingine. Borrell anasema hitilafu hizi ni matokeo ya tofauti kubwa za kitamaduni na kisiasa kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na kuongeza kuwa: Baadhi ya wanachama wa Umoja wa Ulaya wanapinga suala la kuwapokea wahamiaji na kuwa zinafuata sera kama ya Japan zikisema kwamba hazitaki kuwapokea wageni na wahamiaji na kuchanganyika nao, na kwamba zinataka kulinda usafi wa mbari zao. Hata hivyo anasisitiza kuwa, ukuaji wa idadi ya watu barani Ulaya umedumaa na watu wake wanaozeeka wanahitaji sana kuongeza nguvu kazi. Borrell anasema: "Tuna ongezeko dogo la watu katika jamii na kwa sababu hiyo tunahitaji wahamiaji ili tusikabiliane na matatizo katika masuala ya rasilimali watu." 

Wakimbizi waliokwama kwenye mipaka ya nchi za Ulaya

Kupanuka kwa mzozo wa wahajiri na migogoro mingine ya kiuchumi na kisiasa, kumeufanya Umoja wa Ulaya ukabiliwe na changamoro nyingi katika miaka ya hivi karibuni na kuchochea tofauti kati ya wakuu wa nchi za bara hilo. Kughafilika na kutoona mbali kwa nchi za Magharibi kumezidisha athari mbaya za kijamii kwa wakimbizi na wahajiri haramu kutoka Afrika na Asia Magharibi, na matatizo ya watu wanaokimbia vita na umaskini wanaotangatanga katika hali mbaya zaidi katika nchi za Ulaya. Vilevile kutumiwa kisiasa mzozo wa wahamiaji na nara za kijipatia umaarufu, haswa zinazotolewa na harakati na vyama vya mrengo wa kulia vyenye misimamo mikali kwa ajili ya kupata madaraka, kumesababisha hofu ya umma na kueneza hisia za kupinga wahamiaji katika jamii za Ulaya, ikiwemo na Ujerumani kama nchi muhimu zaidi inayowapa hifadhi wahajiri.

Mizizi ya mgogoro wa wahamiaji barani Ulaya inarejea katika sera za kinafiki na kindumakuwili za Wazungu kuhusu suala la mapambano dhidi ya ugaidi na umaskini. Kwa ujmla ni kwamba, Ulaya ina rekodi mbaya katika kushughulikia suala la wahamiaji haramu na wakimbizi. Wakati huo huo, kuendelea kwa mgogoro wa wanaotafuta hifadhi na wahamiaji haramu, pamoja na misimamo inayokinzana ya nchi za Umoja wa Ulaya katika uwanja huu, ambayo ni pamoja na marufuku ya kuingia wahajiri katika nchi hizo, vimelifanya suala hilo kuwa changamoto kubwa kwa Umoja wa Ulaya. Martin Pluim, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema: Mgogoro wa wakimbizi unaonekana kuwa mgogoro wa usimamizi na sera wa Ulaya zaidi kuliko kuwa mgogoro wa idadi kubwa ya wakimbizi wanaoingia barani humo.

Bunge la Ulaya

Kwa sasa pengo na hitilafu kati ya nchi za Umoja wa Ulaya kuhusu namna ya kukabiliana na tatizo la wahajiri zimefikia kiwango ambacho hata Josep Borrell, ambaye ni Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya, ameonya kuhusu madhara yake makubwa hasa uwezekano wa kusambaratika na hatimaye kuvunjwa kwa taasisi hiyo ya Ulaya.

Tags