Msimamo wa China unaokinzana na Wazayuni kuhusu mgogoro wa Gaza
Tangu siku za mwanzo kabisa za shambulio la kasi ya radi la Hamas dhidi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, msimamo wa China kuhusu suala hilo haukuziridhisha Marekani na Wazayuni.
Shambulio hilo la Kimbunga cha al Aqsa, lilitekelezwa wakati ambapo timu ya maseneta wa Marekani wakiongozwa na Chuck Schumer ilipokuwa safarin mjini Beijing ambapo msimamo wa China kuhusu shambulio la kasi ya umeme la Hamas dhidi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ulikosolewa na seneta huyo kwamba ni kwa nini China haiwaungi mkono Wazayuni.
Wakati huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilitoa wito kwa pande mbili za Hamas na Wazayuni kuzuia vita. Wang Yi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China alisema suala la Palestina ndio kiini cha migogoro katika Mashariki ya Kati, na kusisitiza kuwa, suala kuu ni kunyimwa haki za kimsingi watu wa Palestina.
Msimamo huo wa China uliwavunja moyo Wazayuni. Yong, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema kuhusiana na jambo hilo kuwa: Wazayuni wanatarajia kuungwa mkono na kila mtu katika shambulio la Hamas dhidi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hii ni katika hali ambayo katika miaka ya hivi karibuni, haki za watu wa Palestina hazikuheshimiwa hata kidogo na Wazayuni pamoja na wafuasi wao wamekuwa wakijaribu kuwakandamiza na kuwadhulumu Wapalestina ili wakae kimya.
Kwa kuzingatia ukweli muhimu kwamba nguvu ya Marekani inazidi kudidimia na nguvu ya kimataifa imeanza kuelekea Mashariki, Wazayuni hawawezi tena kutarajia China na madola mengine ya Mashariki kuitikia matakwa ya Wazayuni kuhusiana na operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa. Nchi za Mashariki zenyewe zina maoni na misimamo yao huru juu ya suala la Ghaza na zinaweza kuamua na kutangaza misimamo hiyo kuhusu Palestina nje ya maoni na matakwa ya Wazayuni na waungaji mkono wake. Ni kutokana na ukweli huo ndio viongozi wa Marekani na Utawala wa Kizayuni wakaonyesha kutoridhishwa kwao na msimamo wa China na madola mengine ya Mashariki kuhusiana na shambulizi la Hamas dhidi ya Isreal na wakalichukulia jambo hilo kuwa ni kuimarisha nguvu na uwezo wa kundi hilo la wanamapambano wa Palestina dhidi ya Wazayuni.
Amin Farjad, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema, China daima inapinga vitendo vinavyodhuru raia na kukiuka sheria za kimataifa.
Msimamo huo wa kibinadamu na wa kuheshimu sheria za kimataifa wa China ni mzito kwa Wazayuni na waungaji mkono wao, na ndio maana hawaukubali kabisa. Hii ni katika hali ambayo msimamo wa China hauwaungi mkono Wapalestina, bali unatilia mkazo suala la kuheshimiwa sheria na kukomeshwa mauaji ya raia yanayofanywa na Wazayuni, jambo ambalo haliendani na matakwa ya Wazayuni.
Kwa vyovyote vile, baada ya takriban miongo saba ya kukalia kwa mabavu ardhi za Waplestina, Wazayuni walidhani kwamba chini ya siasa za Marekani, hususan baada mpango unaodaiwa kuwa wa amani wa Abraham, wangeweza kujiimarisha kieneo na kimataifa, lakini uungaji mkono wa kimataifa kwa operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa na kulaaniwa vikali mauaji ya raia unaofanywa na Wazayuni, umeonyesha kwamba ulimwengu bado unapinga kuwepo dola la kisiasa linaloitwa Israel, na kwamba Wazayuni hao watenda jinai kamwe hawatamiliki ardhi ya Palestina, na wala dunia haitalitambua rasmi dola hilo ghasibu. Kwa msingi huo si Wazayuni tu bali Wamarekani pia hawaridhishwi hata kidogo na misimamo ya China kuhusu kadhia ya Gaza, na hili linathibitika wazi kwa msimamo huo huru, madola ya Mashariki ikiwemo China yako kwenye mkondo unaofaa na yamesimama upande sahihi wa historia.