Dec 10, 2023 05:54 UTC
  • Radiamali ya China kuhusu kura ya turufu ya Marekani dhidi ya azimio la kusitisha vita Gaza

Zhang Jun, mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, ameitaja kura ya turufu ya Marekani dhidi ya azimio la kusitisha mapigano huko Gaza kuwa imeweka wazi siasa za kundumakuwili za Washington katika uwanja wa kimataifa.

Ukweli wa mambo ni kwamba jamii ya kimataifa inataka kusimamishwa mara moja jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza, lakini Marekani imeutaka utawala wa Kizayuni uendeleze jinai hizo na kwa hivyo ilitarajiwa kuwa ingechukua hatua ya kuaibisha ya hivi karibuni ambayo imekwenda kinyume kabisa na matakwa ya waliowengi kuhusiana na jambo hilo.

Jeshi la utawala wa Kizayuni limekuwa likishambulia kinyama Ukanda wa Gaza tangu tarehe 7 Oktoba, lakini licha ya mauaji makubwa yanayofanyika dhidi ya raia wa Gaza ambayo kufikia sasa yamepelekea zaidi ya watu elfu 17 kuuawa shahidi na wengine zaidi ya elfu 46 kujeruhiwa, lakini bado haujafikia malengo uliyoyatangaza rasmi muhimu zaidi ikiwa ni kulitokomeza kundi la muqawama wa Kiislamu wa Palestina Hamas.

Mwakilishi wa Marekani apinga azmio la kusimamisha vita Gaza

Abolfazl Zahrawand, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Lengo la kura ya turufu ya Marekani dhidi ya azimio la kusimamisha vita na jinai za Wazayuni huko Gaza ni kutoa fursa ya kujipatia mafanikio ya kijeshi utawala huo. Zaidi ya miezi miwili imepita tangu kuanza jinai za Wazayuni huko Gaza na utawala huo haujapata mafanikio yoyote katika malengo yake na unazidisha faili la jinai zake za kivita huko Gaza. Kwa hivyo, Marekani imetoa fursa ya wiki kadhaa kwa Wazayuni kufikia malengo hayo.

Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotaka kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza liliungwa mkono na zaidi ya nchi 100 pamoja na wanachama 13 kati ya 15 wa Baraza la Usalama. Lakini Marekani, ambayo inaendeleza siasa zake za kundumakuwili kuhusu Gaza, imepinga kwa kiburi azmio hilo na kuuthibitishia ulimwengu kuwa ni muungaji mkono mkuu wa utawala katili na gaidi wa Kizayuni.

Kwa hivyo, Mwakilishi wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa amekanusha madai ya Marekani ya kujali maisha ya binadamu katika Ukanda wa Gaza. Kwa mujibu wa Zhang Jun, azimio lililopendekezwa na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa niaba ya nchi za Kiarabu liliakisi ombi la jamii ya kimataifa na mwelekeo sahihi wa kurejesha amani katika eneo hilo, na China inaunga mkono kikamilifu suala hilo.

Kikao cha Baraza la Usalama

Hata hivyo Marekani kwa kupinga fikra za waliowengi duniani inafuatilia kwa nguvu zake zote ushindi wa utawala wa Kizayuni ambao katika kipindi cha miezi miwili iliyopita umeshindwa kufikia malengo yake dhidi ya wakazi wa Gaza jambo ambalo limezidisha maandamano ya kila siku dhidi ya Netanyahu Waziri Mkuu mhalifu na mtenda jinai wa Kizayuni ndani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Zhong Yun Tso, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema kuhusu suala hilo: Marekani imetumia heshima na hadhi yake yote kwa ajili ya kufanikisha juhudi za Israel huko Gaza, lakini ukweli wa mambo ni kuwa wanaharakati wa mapambano wa Kipalestina wanakabiliana vilivyo na wanajeshi wa Isreal na inaonekana kuwa suala hilo limeikasirisha Marekani zaidi kuliko Wazayuni wenyewe, ambapo Washington inajaribu kuvuta wakati kadiri inavyowezekana ili kumnusuru Netanyahu na kumuwezesha kujikwamua kutoka kwenye kinamasi alichokwama ndani huko Gaza.

Kwa vyovyote vile, mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa ambaye nchi yake imechukua uongozi wa zamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ameitaka Israel kutilia manani matakwa ya jumuiya ya kimataifa na kusimamisha vita haraka iwezekanavyo kwa kuzingatia hasara na uharibifu mkubwa unaosababishwa na mashambulizi ya anga na makombora huko Gaza. Inaonekana China na nchi nyingine zinapaswa kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya Wazayuni, ikiwa ni pamoja na kukata mahusiano na Israel na kusimamisha kuutumia bidhaa muhimu. Katika hali hiyo tunaweza kuwa na matumaini ya kukomeshwa jinai za Wazayuni huko Ghaza. Vinginevyo, utawala huo utaendeleza jinai zake dhidi ya wananchi wasiokuwa na hatia wa Gaza kwa himaya ya Marekani.

Hii ni katika hali ambayo, hakuna matumaini ya ushindi wa Wazayuni dhidi ya matakwa ya watu wa Gaza, na kushambuliwa watu wasio na ulinzi wala zana za kijeshi hakuwezi kuchukuliwa kuwa ni mafanikio ya kijeshi kwa Israel.

 

Tags