Maafisa 5 wa polisi wauawa katika mripuko Pakistan
Maafisa wa polisi wasiopungua watano wameuawa na karibu wengine 24 kujeruhiwa baada ya gari yao kukumbwa na mripuko wakati wakiimarisha ulinzi katika zoezi la utoaji chanjo za polio huko kaskazini magharibi mwa Pakistan.
Maafisa wa Pakistan wameiambia televisheni ya al Jazeera kuwa mripuko huo tajwa ulitokea leo asubuhi huko Bajaur, wilaya ya kikabila katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa karibu na Afghanistan; wakati Pakistan ikiwa imeanzisha duru ya utoaji chanjo ya polio kwa watoto nchini.
Bilal Faizi Msemaji wa huduma za uokoaji katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa amesema kuwa polisi watano kati ya majeruhi wana hali mbaya na tayari wamehamishwa huko Peshawar makao makuu ya jimbo hilo umbali wa kilomita 133 kusini mwa Bajaur. Hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na mripuko wa leo huko Bajaur Pakistan.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, katika miaka ya hivi karibuni kundi la Taliban la Pakistani linalojulikana kwa kifupi kwa jina la TTP limehusika katika mauaji ya makumi ya wafanyakazi wa chanjo ya polio na maafisa wa usalama huko Pakistan.
Upinzani dhidi ya mpango wa utoaji chanjo ya polio uliongezeka huko Pakistan baada ya Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kuandaa zoezi la uwongo la utoaji chanjo nchini humo kwa lengo la kumnasa Osama bin Laden ambaye aliuawa katika mji wa Abbottabad mwaka 2011.
Aidha viongozi wa kidini katika eneo la mpaka wa Pakistan na Afghanistan pia walieneza habari potofu kwamba chanjo hiyo ilikuwa na chembechembe za nyama ya nguruwe na pombe, ambazo ni haramu katika Uislamu. Pakistan na Afghanistan ni nchi mbili pekee ambazo hadi sasa hazijatangaza kuwa hazina ugonjwa wa polio unaoambukizwa na virusi aina ya WPV-1.
Ili nchi iweze kutambuliwa kutokuwa na ugonjwa wa polio inapasa kuthibisha kutokuwa na maambukizi ya maradhi hayo kwa miaka isiyopungua mitatu mfululizo. Hii ni kwa mujibu wa Mpango wa Kimataifa wa Kutokomeza Polio.