Jan 28, 2024 13:28 UTC
  • Maelfu waandamana Madrid kuliunga mkono taifa la Palestina

Maelfu ya wananchi wa Uhispania kwa mara nyingine tena wamemiminika katika barabara za mji mkuu wa nchi hiyo, Madrid kutangaza uungaji mkono wao kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina hasa wa Ukanda wa Gaza, na vilevile kulaani mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala haramu wa Israel katika ukanda huo.

Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, maelfu ya watu walijitokeza katika mitaa na barabara za Madrid kushiriki maandamano hayo ya kuiunga mkono Palestina, ambapo sambamba na kutangaza mshikamano wao na watu wa Gaza wamelaani pia mauaji ya kimbari ya utawala bandia wa Israel.

Maandamano hayo yamevutia wanaharakati wa mashirika mbalimbali ya kiraia na vyama tofauti vya siasa kama vile wafuasi wa Chama cha Uhispania cha United Left (IU). Aidha Waziri wa Vijana wa nchi hiyo, Sira Rego ni miongoni mwa shakhsia wa kisiasa walioshiriki maandamano hayo.

Waandamanaji hao mjini Madrid waliokuwa wamebeba bendera za Palestina wamemtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Pedro Sanchez kutangaza mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza kuwa ni mauaji ya kimbari sambamba na kuiwekea Tel Aviv vikwazo vya silaha.

Mwishoni mwa mwezi uliopita pia, wanaharakati kutoka mamia ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini Uhispania walifanya maandamano na kukusanyika nje ya Bunge la nchi hiyo, wakiitaka serikali yao isimamishe bishara ya silaha na utawala haramu wa Israel.

Wahispania walioshiriki kwa wingi maandamano hayo ya jana Jumamosi mjini Madrid walitoa wito wa kusitishwa mara moja vita vya maangamizi ya umati vya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza. Bango moja lililokuwa limebebwa na waandamanaji hao lilikuwa na ujumbe unaosema: Mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina Gaza ni mauaji ya kimbari.

Utawala katili wa Israel umekuwa ukishambulia na kulipua kwa mabomu eneo hilo linalozingirwa kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, ili kulipiza kisasi cha shambulizi la kushtukiza la Kimbunga cha al-Aqsa la Oktoba 7 mwaka jana.

Tags