Mar 05, 2024 07:42 UTC
  • Kuongezeka uungaji mkono wa wananchi wa Marekani kwa Wapalestina

Matokeo ya uchunguzi wa maaoni uliofanywa na jarida la Wall Street Journal yanaonyesha kuwa, wananchi wengi wa Marekani hawaridhishwi na utendaji kazi wa Rais Joe Biden katika vita vya Gaza.

Wamarekani hao wanaamini kwamba, utawala wa Kizayuni ulichukua hatua kubwa kupita kiasi katika kukabiliana na operesheni ya kimbunga ya Al-Aqswa ya tarehe 7 Oktoba. Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni wa Wall Street Journal uliofanyika kuanzia Februari 21 hadi 28 yanaonyesha kwamba, umma wa Marekani siku baada ya siku unawahurumia na kuwa pamoja nao Wapalestina huko Gaza na raia waliopoteza makazi yao na kufurushwa makazi yao kutokana na mashambulizi ya Wazayuni.

Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni yanaonyesha kwamba takriban asilimia 42 ya walioshiriki wanaamini kuwa, Israel imechupa mipaka katika mashambulizi yake huko Gaza. Asilimia 19 wanaamini kwamba, Israel inapaswa kuchukua hatua zaidi; na aslimia 24 wanasema kuwa, jibu la Israel kwa HAMAS lilikuwa la kutosha na lenye uwiano.

Katika uchunguzi mwingine wa maoni uliofanywa nchi nzima huko Marekani mwishoni mwa Januari 2024, ilibainika kuwa nusu ya Wamarekani wanaamini kuwa, utawala wa Kizayuni unafanya mauaji ya halaiki huko Gaza.

Inaonekana kuwa, kuendelezwa vita vya Gaza na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuongezeka idadi ya mashahidi na majeruhi Wapalestina wanaoishi Gaza ambayo imepindukia watu 100,000, kumepelekea hata watu wengi wa Marekani inayohesabiwa kuwa mshirika wa kistratijia wa Israel kujitokeza na kukosoa mtambo wa mauaji wa utawala wa Kizayuni unaoendelea kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Gaza kwa mwezi wa tano sasa. Aidha, maandamano mengi yamekuwa yakifanyika katika miji tofauti ya Marekani kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza.

Watoto wa Kipalestina wakisubiri chakula cha msaada

 

Juzi mamia ya watu waliandamana na kukusanyika mbele ya ubalozi wa Israel mjini Washington, Marekani kulaani vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Nukta muhimu ni kwamba, licha ya msimamo wa Rais wa sasa Joe Biden na serikali yake wa uungaji mkono wa bila masharti na wa pande zote kwa Israel na kufanya jitihada za kuwalaumu Wapalestina hususan Harakati ya HAMAS kwa kuanzisha vita vya sasa vya Gaza, lakini hata wanasiasa wa Marekani, wanafahamu vyema utambulisho wa kivamizi na kichokozi wa utawala wa Kizayuni na ukandamizaji wa miongo kadhaa wa Wazayuni dhidi ya Wapalestina ambao umeendelea hadi hivi sasa kwa kuua na kupora ardhi zao na hivyo wamejitokeza hadharani na kukosoa jambo hilo.

Katika uwanja huo, Jeff Merkley, mjumbe wa chama cha Democratic katika Baraza la Seneti la Marekani amesisitiza kuwa, Marekani inahusika katika baa la njaa na maafa ya kibinadamu huko Gaza na kuutaka utawala wa Biden kujitenga na utawala wa Kizayuni na kupeleka misaada moja kwa moja katika Ukanda wa Gaza. Jack Reed, Mwenyekiti wa Kamati ya Vikosi vya Usalama katika Baraza la Seneti la Marekani na Seneta Angus King, mjumbe wa kamati hiyo, naye amemtaka Rais wa Marekani kutuma haraka iwezekanavyo meli ya jeshi ya huduma za hospitali katika Ukanda wa Gaza ili kudhamini kuwasili kwa msaada wa matibabu kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza.

 

Kuongezeka shinikizo la ndani la watu, baadhi ya taasisi na baadhi ya wanasiasa wa Marekani dhidi ya utawala wa Biden kwa upande mmoja, na wasiwasi mkubwa juu ya kupoteza kura za wafuasi wa Rais Biden katika uchaguzi ujao wa Novemba mwaka huu (2024) na kumtelekeza Biden kwa upande wa pili, ni jambo ambalo limepelekea maafisa wakuu wa Washington nao wajitokeze na kutaka kufanyika mabadiliko angalau ya kidhahiri kuhusiana na hali mbaya ya Gaza.

Kuhusiana na suala hilo, Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris ameyataja mazingira ya Ukanda wa Gaza kuwa si ya kibinadamu na kusisitiza juu ya udharura wa kusitishwa vita mara moja katika Ukanda huo. Aidha ameutaka utawala wa Kizayuni kuruhusu misaada zaidi kuingia katika eneo hilo "bila ya visingizio vyovyote".

Nukta muhimu ni hii kwamba, pamoja na kuwa serikali ya Biden imekuwa ikitaka mara kwa mara kubadilishwa hali ya mambo huko Gaza na kupelekwa misaada kwa watu wanaodhulumiwa wa eneo hilo, lakini haijaweka shinikizo lolote kubwa kwa Tel Aviv na hata imeendelea kuutumia utawala huo silaha ili kuendeleza hujuma na mashambulio dhidi ya Gaza.

Fauka ya hayo, katika madai ya kushangaza, serikali ya Biden imekanusha kutokea mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza ilihali asasi za kieneo na kimataifa pamoja na tathmini mbalimbali zimethibitisha hilo.  

Hapana shaka kuwa, kuendelea utendaji wa sasa wa serikali ya Biden kuhusiana na vita vya Gaza sambamba na uungaji mkono wake kwa utawala wa Kizayuni wa Israel utapelekea kupungua kwa kura za Joe Biden katika uchaguzi ujao wa urais wa Marekani kutoka kwa wafuasi kindakindaki wa chama cha Democratic.

Tags