Uchunguzi wa maoni: 'Demokrasia ya Marekani' inaleta machafuko duniani
Uchunguzi mpya wa maoni umebaini kuwa migogoro na majanga mengi duniani yanatokana na sera ya Marekani ya kueneza kile inachodai kuwa ni 'demokrasia" duniani.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na televisheni ya China ya CGTN kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Renmin cha China na Taasisi ya Mawasiliano ya Kimataifa ya New Era, waliohojiwa duniani walionyesha kiwango cha juu cha kutoridhishwa na kuendelea Marekani kutumia suala la demokrasia kukandamiza nchi nyingine kwa manufaa yake binafsi, na vilevile kuzidisha mgawanyiko wa dunia na migogoro.
Kulingana na uchunguzi huo, asilimia 71 ya waliohojiwa waliikosoa Marekani kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kuzikandamiza chini ya kisingizio cha "demokrasia. Wakati huo huo, asilimia 62.3 ya waliohojiwa walionyesha kutoridhishwa na tabia ya Marekani ya ubeberu" na kutumia vibaya vikwazo na kulazimisha nchi zifuate sera zake za kiuchumi.

Katika uchunguzi huo, karibu asilimia 70 (asilimia 68) ya waliohojiwa duniani wana wasiwasi sana kuhusu historia ndefu ya Marekani ya kuchochea "mapinduzi ya rangi" na kuendesha "vita vya niaba" kote ulimwenguni. Asilimia 65.8 ya waliohojiwa walipinga vikali kulazimisha nchi nyingine kubadili mifumo yao ya kisiasa kupitia mapinduzi ya serikali zilizoko madakarani na uvamizi.
Kulingana na kura ya maoni, asilimia 84.3 ya waliohojiwa wanaamini kuwa demokrasia inajidhihirisha kwa njia mbalimbali katika nchi na tamaduni tofauti. Aidha wengi wanaamini kuwa hakuna anayeweza kudai kuwa kielelezo bora cha demokrasia na haiwezekani kuwa na mfumo wa kisiasa wa aina moja.
Asilimia 84.8 ya waliohojiwa wana maoni kwamba wakati wa kuamua juu ya mfumo wa kisiasa, nchi inapaswa kuzingatia historia, utamaduni na hali ya kitaifa. Asilimia 79.5 ya waliohojiwa walionyesha upinzani mkali dhidi ya ubeberu na utumiaji mabavu Marekani katika kiwango cha kimataifa chini ya bendera ya "demokrasia."
Asilimia 86.8 ya waliohojiwa waliitaka Marekani kukomesha ubeberu wake wakati wa maingiliano na nchi nyingine.