Mwaka 2023 ulivunja rekodi zote za joto duniani
Mwaka 2023 ulikuwa mwaka wenye joto zaidi duniani katika rekodi zote zilizowahi kunukuliwa, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa duniani, WMO katika ripoti yake iliyotolewa Jumanne huko Geneva, Uswisi.
Mwaka 2023 ulikuwa mwaka wenye joto zaidi duniani katika rekodi zote zilizowahi kunukuliwa, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa duniani, WMO katika ripoti yake iliyotolewa Jumanne huko Geneva, Uswisi.
Taarifa ya WMO kutoka Geneva imesema: “Rekodi zimevunjwa, katika baadhi ya maeneo kwa kiwango kikubwa katika viwango vya hewa chafuzi, viwango vya joto ardhini, viwango vya juu vya tindikali na joto baharini, ongezeko la kiwango cha maji ya bahari na kupungua kwa barafu na theluji huko ncha ya kusini mwa dunia au Antarctic.”
Kama hiyo haitoshi mikondojoto baharini, mafuriko, ukame, mioto ya nyika na kasi kubwa ya vimbunga kwenye maeneo ya kitropiki vyote vimesababisha zahma na machungu na kuweka rehani maisha ya mamilioni ya watu, huku nazo nchi zikikumbwa na hasara za kiuchumi za mabilioni ya dola.
Kiwango cha joto mwaka 2023 kwa wastani kiliongezeka kwa wastani wa nyuzi joto 1.45 katika kipimo cha Selsiyasi ikilinganishwa na kabla ya mapinduzi ya viwanda. Ulikuwa ni mwaka wa kumi mfululizo kwa kiwango cha juu cha joto, imesema ripoti hiyo
Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo ametoa indhari kwa dunia na kuongeza kuwa: “Kamwe hatujawahi kukaribia kabisa angalau kwa sasa kiwango cha nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kwa ambacho hatupaswi kuvuka kwa mujibu wa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.”
Joto la bahari liliharibu mifumo anuai na ile ya uzalishaji chakula. Mwishoni mwa mwaka 2023, asilimia 90 ya eneo la baharí katika kipindi fulani lilikumbwa na mazingira ya mikondo joto.
Katibu Mkuu huyo wa WMO anasema janga la tabianchi ndio changamoto inayokumba ubinadamu hivi sasa na inaenda sambamba na ukosefu wa usawa kutokana na ongezeko la ukosefu wa uhakika wa chakula, ukimbizi na upotevu wa bayonuai.
Aidha idadi ya watu wasio na chakula imeongezeka maradufu kutoka milioni 149 kabla ya COVID-19 hadi milioni 333 mwaka 2023 kwenye nchi 78 ambazo zinafuatiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP.